1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BRUSSELS: Urusi na Belarus zatakiwa zitoe maelezo

8 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCcG

Halmashauri ya Umoja wa Ulaya imeitaka Urusi na Belarus zieleze mara moja kwa nini usafirishaji wa mafuta kutoka Urusi kwenda Poland na mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya umesitishwa.

Maofisa nchini Poland wameripoti kwamba usafirishaji wa mafuta ya petroli kutoka Urusi kwenda Poland na Ujerumani umesimamishwa katika mpaka wa mashariki mwa Poland na Belarus. Haijabanikia wazi ikiwa hatua hiyo imechukuliwa na serikali mjini Minsk au na kampuni ya kusafirisha mafuta ya Transneft ya Urusi.

Hatua hiyo ni sehemu ya mgogoro kati ya Urusi na Belarus juu ya matumizi ya bomba la mafuta la Druzhba. Mwanzoni mwa mwaka huu, Belarus iliongeza kodi inayotozwa mafuta ya Urusi yanayopitia ardhi yake kwenda mataifa mengine ya Ulaya.

Uamuzi huo ulichukuliwa kufuatia hatua ya Urusi kuondoa ruzuku kwa mafuta yanayonunuliwa na Belrausu kutoka Urusi. Urusi inasafirisha asilimia 20 ya kiwango cha mafuta ya petroli kinachotumiwa nchini Ujerumani.

Mpaka sasa serikali mjini Berlin haijatoa ripoti yoyote kuhusu kukatizwa kwa usafirishaji huo wa mafuta.