1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BRUSSELS : Wataka mkutano licha ya mzozo wa Zimbabwe

21 Septemba 2007
https://p.dw.com/p/CBNm

Mkutano wa kihistoria wa viongozi wa Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika hapo mwezi wa Desemba haupaswi kushikiliwa mateka na mzozo kati ya Uingereza na Zimbabwe juu ya ushiriki wa Rais Robert Mugabe.

Msemaji wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Johannes Laitenberger amewaambia waandishi wa habari waanaamini kwamba uhusiano kati ya Ulaya kwa jumla na Afrika haupaswi kushikiliwa mateka na hali mahsusi.

Amesema wanakubaliana na mashtaka ya Uingereza na ya Waziri Mkuu Gordon Brown juu ya hali ya Zimbabwe na kwamba bila ya shaka wana nia ya kukabiliana na hali hiyo ambayo ni ya wasi wasi sana.

Hapo jana Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown amependekeza vikwazo vipya dhidi ya Zimbabwe na kutishia kususia mkutano huo wa viongozi wa Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika uliopangwa kufanyika nchini Ureno iwapo Rais Robert Mugabe atahudhuria mkutano huo.

Brown amempongeza Waziri Mkuu wa Ureno kwa kile anachojaribu kufanya kujenga uhusiano madhubuti kati ya Ulaya na Afrika.

Amesema huu ni mkutano wa viongozi ambao ni muhimu kwa maslahi ya Afrika lakini bila ya shaka litakuwa jambo lilisilofaa kabisa kwake yeye kuwepo kwenye mkutano huo iwapo Rais Mugabe atakuwepo kwa sababu rais huyo anakusudia kwenda kwenye mkutano huo.

Mkutano huo unatazamiwa kuwakutanisha pamoja zaidi ya viongozi 70 wa nchi na serikali mjini Lisbon tarehe nane na tisa mwezi wa Desemba.