1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brussels yakosa muafaka mgogoro wa wakimbizi

Admin.WagnerD15 Septemba 2015

Mawaziri wa mambo ya ndani wa Umoja wa Ulaya wameshindwa kuafikiana kuhusu mpango wa kugawana wakimbizi wanaozidi kumiminika barani humo, huku mataifa mengine yakianzisha ukaguzi wa mipakani.

https://p.dw.com/p/1GWev
Mawaziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani Thomas de Maiziere, na Ufaransa Bernard Cazeneuve wakizungumza na wandishi habari mjini Brussels.
Mawaziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani Thomas de Maiziere, na Ufaransa Bernard Cazeneuve wakizungumza na wandishi habari mjini Brussels.Picha: picture-alliance/AP Photo

Wakati ambapo kanda ya usafiri huru ya Schengeni iliyodumu kwa miaka 20 ikikiwa chini y ashinikizo kubwa, Austria na Slovakia zilisema jana kuwa zinafuata nyayo za Ujerumani kurejesha ukaguzi wa mipakani ili kuweza kushughulikia mmiminiko wa watu. Poland ilisema inatafakari hatua sawa, huku Uholanzi ikisema itaongeza doria kwenye mipaka yake.

Misururu mirefu ya magari ilishuhudiwa kwenye mpaka wa Ujerumani na Austria, huku wakimbizi wakiachwa wamekwama katika upande wa Serbia katika mpaka wake wa na Hungary, katika matukio ya karibuni ya vurugu zinazotokana na mgogoro mkubwa zaidi wa wakimbizi tangu kumalizika kwa vita kuu vya pili vya dunia.

Na huku kukiwa na upinzani mkali kutoka mataifa ya Ulaya Mashariki, mawaziri wa Umoja wa Ulaya walishindwa kuafikiana juu ya mpango wa kugawana wakimbizi 120,000 ili kuyapunguzia mzigo mataifa yalioko kwenye mipaka wanakoingilia wakimbizi hao wanaokimbia vita.

Wakimbizi wakiwa wamekwama kwenye mpaka wa Serbia na Hungary.
Wakimbizi wakiwa wamekwama kwenye mpaka wa Serbia na Hungary.Picha: Reuters/L. Balogh

"Hatukuweza kupata msimamo wa pamoja. Hii ni kutokana kwa sehemu na mikataba ya Umoja wa Ulaya, ambayo inahitaji baadhi ya maamuzi kufanywa kwa wingi wa kura. Tulijaribu kutafuta muafaka na tumejitahidi kupata matokeo ya pamoja lakini bahati mbaya hili halikuwezekana," alisema Thoma de Maiziere, waziri wa mambo ya ndani ya Ujerumani baada ya mkutano wa mjini Brussels.

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Bernard Cazeneuve, aliyakosoa mataifa yanayoendelea kupinga mpango huo, na kuyakumbusha kuwa Ulaya ni bara la mshikamano. "Mataifa kadhaa hayataki kuheshimu mchakato huu wa mshikamano, na hayo hasa ni mataifa ya kundi la Visegrad - yaani Jamhuri ya Czech, Hungary, Poland na Slovakia, na Ufaransa inapenda kuwa wazi kabisaa kwamba mshikamano haugawanywi," alisema waziri Cazeneuve.

"Mzigo wa wakimbizi hauwezi kuziangukia nchi tano tu zinazochukuwa asilimia 75 ya wanaotafuta hifadhi. Na iwapo Ulaya inataka kutimiza matarajio ya umma kutokana na mtihani wake wa kiutu, basi mataifa yote laazima yatimize wajibu wao," aliongeza waziri huyo wa mambo ya ndani wa Ufaransa.

Umoja wa Ulaya wazidiwa kasi

Kamishna wa uhamiaji wa Umoja wa Ulaya Dimitris Avramopoulos, alisema baada ya mkutano huo wa dharura mjini Brussels, kuwa wanatumaini makubaliano yanaweza kufikiwa mwezi Oktoba.

Lakini mgogoro huo unakwenda kasi kuliko Umoja wa Ulaya unavoyweza kushughulikia, ambapo mpaka sasa zaidi ya watu 430,000 wamevuka bahari ya Meditarrani mwaka huu, 2,748 wamengamia katika bahati hiyo na wengine zaidi wanakuja kila siku.

Shirika la haki za binaadamu la Amnesty International limekosoa kushindwa kupatikana kwa muafaka, likisema kwa mara nyingine mawaziri wa Umoja wa Ulaya wameshindw akuonyesha uongozi wa pamoja na kushughulikia mgogoro huu wa kimataifa.

Wakimbizi wakisubiri mabasi mjini Nickelsdorf mapakani mwa Austria na Hungary.
Wakimbizi wakisubiri mabasi mjini Nickelsdorf mapakani mwa Austria na Hungary.Picha: picture-alliance/dpa/H. Oczeret

Baada ya kukosekana kwa mufaka, waziri Thoma de Maiziere, amesema katika mahojiano na shirika la utangazaji la ZDF la hapa Ujerumani, kuwa ipo haja ya kuyawekea mataifa shinikizo kukubali mgawanyo wa wakimbizi kwa kutumia ufadhili wa Umoja wa Ulaya, kwa sababu mataifa yanayokataa hasa mgawanyo huo yanapokea ufadhili mkubwa wa maendeleo ya miundombinu kutoka umoja huo.

Wengine wazama wakielekea Ugiriki

Wakati huo huo, vyombo vya habari Uturuki vimeripoti kuwa wahamiaji 22 waliokuwa wanajaribu kwenda nchini Ugiriki kwa kutumia boti, wakiwemo wanawake 11 na watoto wanne, wamefariki baada ya boti hiyo kuzama nje ya pwani ya kusini mwashariki mwa Uturuki.

Askari wa ulinzi wa pwani wa Uturuki wamewaokoa wahamiaji 211 kutoka kwenye boti hiyo iliyotengeneza kwa mbao, ambayo iliondokea mji wa mapumziko wa Datca kusini-magharibi, kuelekea kisiwa cha Kos, kulingana na shirika la habari la Dogan.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman