1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bujumbura yatumia taka kuzalisha nishati.

Sekione Kitojo2 Juni 2007

Miezi kadha iliyopita , wakaazi wa mji mkuu wa Burundi , Bujumbura, walikuwa wakihangaika jinsi ya utupaji taka kutoka majumbani mwao. Huduma ya ufundi ya jiji la Bujumbura haikuwa na njia ya kushughulikia utupaji wa taka zote ngumu, na hali ya afya katika mji huo ilikuwa inaporomoka. Lakini ilipokaribia Juni 2007, mambo yameanza kubadilika, hii inatokana na hatua za kushughulikia taka ngumu, zilizoazimwa kutoka nchi jirani ya Rwanda na kutumika hivi karibuni na kundi la maendeleo na kupambana na umasikini.

https://p.dw.com/p/CHkj

Shirika hilo limejitokeza baada ya maafisa kuamua kufungua milango ya ukusanyaji wa taka ngumu na ushughulikiaji wa maji taka kwa wakandarasi kutoka nje, na kuwa shirika la kwanza linalomilikiwa kibinafsi kuhusika katika kazi ya kushughulikia taka katika mji huo.

Alidi Hakizimana , mkaazi wa eneo la Nyakabiga katikati ya mji wa Bujumbura , ambako shirika hilo la ADLP, linashughulika , anadokeza kuwa hali ya kiafya , imeimarika sana tangu shirika hilo lilipochukua jukumu la kushughulikia taka, katika eneo hilo.

Lakini ADLP halikusanyi tu taka , lakini pia linatumia taka hizo kuzalisha nishati.

Taka hizo ambazo kwa kiasi kikubwa ni pamoja na mabaki ya mboga mboga, maganda ya matunda na vifaa vya plastiki, zinakusanywa na shirika hilo, na kukaushwa, kisha huwekwa katika mashine na kuzalisha matofali makubwa yenye rangi ya kijivu.

Matofali ya mwanzo ya taka hizo yalianza kutengenezwa August mwaka jana , na yamekuwa tangu wakati huo yakipewa nguvu kubwa na watu wanaoyatumia kama mkaa.

Josee Ndayisenga , mama wa nyumbani mjini Bujumbura , anasema kuwa matofali hayo ni rahisi kushika moto na hayazimiki moto wake kwa kipindi chote cha kupika. Hii ni nishati ya kuweza kuwapelekea watu masikini, kwa kuwa si ghali, amesema.

Kwa mujibu wa ADLP, nyumba yenye watu 32 ambayo inatumia dola 3 kwa siku kwa ajili ya kuni na mkaa itatumia kiasi cha dola mbili tu iwapo itaanza kutumia nishati inayotokana na taka hizo.

Tarakimu kutoka katika ripoti ya mwaka 2006 ya maendeleo ya jamii, iliyotayarishwa na mpango wa maendeleo wa umoja wa mataifa, inaonyesha kuwa kiasi cha asilimia 55 ya Warundi wanaishi kwa kutumia chini ya dola moja kwa siku.

Hatua hiyo pia imefanikiwa kutengeneza nafasi za kazi kwa baadhi ya wakaazi wasikini wa mjini Bujumbura, kama wajane, vijana na wapiganaji wa zamani ambao wamepigana katika vita vya wenyewe kwa wenyewe , vita vilivyoikumba Burundi katika miaka ya hivi karibuni. Kiasi cha watu 80 katika mji huo hivi sasa wanaishi kutokana na ukusanyaji wa taka,na usafirisaji . Pamoja na hayo matumizi ya matofali haya ya taka badala ya mkaa wa miti unaleta matumaini ya mafanikio ya ulinzi wa mazingira.

Pierre Birampanze, mkurugenzi wa nishati katika wizara ya nishati na madini , anadokeza kuwa Burundi inatumia miti ili kukidhi mahitaji ya asilimia 96.6 ya nishati. Hata hivyo , hatua ya kuchoma mkaa kutokana na miti , unaohitajika kwa ajili ya kupikia pamoja na mambo mengine si ya hakika. Kwa sasa kilo 10 za miti zinahitajika kutoa kiasi cha kilo moja ya mkaa.

Hii inasababisha kupoteza misitu, amesema Astere Bararwandika , mkurugenzi wa misitu , na kuongeza kuwa kiasi cha hekta 2,160 za miti zinaharibiwa kila mwaka kutokana na kukata miti kwa ajili ya mkaa. Matumizi ya matofali hayo yatokanayo na taka yatasaidia kuzuwia uharibifu wa misitu na wa ardhi unaotokana nayo.