1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BUJUMBURA:Waasi wa FNL washambulia polisi wawili

22 Februari 2007
https://p.dw.com/p/CCPf

Wanachama wa kundi la uasi lililobakia nchini Burundi wanashukiwa kuwaua polisi wawili katika shambulio moja kwa mujibu wa maafisa wa serikali.Tukio hilo ni la kwanza kutokea tangu makubaliano ya kusitisha vita kufikiwa mwezi Septemba mwaka jana.Kulingana na msemaji wa waziri wa mambo ya ndani wa Burundi Ildephonse Mushwabure polisi wawili waliuawa na wengine wawili kujeruhiwa katika eneo la Nkenga kusini mashariki mwa mji wa Bujumbura.

Waasi hao walimkatakata mmoja wa maafisa hao wa polisi na kumfunga wa pili kamba miguu na viganja vya mikono kabla kumpiga kwa mawe hadi kufa.

Afisa mmoja wa serikali katika eneo hilo alikamata na kuzuiliwa kwa kushukiwa kuhusika na shambulio hilo.Kulingana na msemaji huyo wa Wizara ya mambo ya ndani tukio hilo linaashiria kuwa shambulio hilo limetekelezwa na kundi la waasi la FNL.

Kundi la waasi la National Liberation Front FNL ndilo kundi la uasi lililosalia nchini Burundi na kujitenga na makubaliano ya amani yaliyofikiwa mwaka 2000.Kundi la FNL lilifanya majadiliano na serikali mwanzoni mwa wiki hii ili kutafuta mbinu ya utekelezaji wa makubaliano ya amani yaliyofikiwa mwaka jana.