1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BUNDESLIGA YAANZA LEO

Ramadhan Ali10 Agosti 2007

Mabingwa Stuttgart wanamenyana leo na makamo-bingwa Schalke katika mpambano wa kwanza kabisa wa msimu mpya.Kesho Bayern munich ina miadi na Hansa Rostock.

https://p.dw.com/p/CHbM

Leo firimbi inalia kuanzisha msimu mpya wa Bundesliga-Ligi ya Ujerumani:mabingwa Stuttgart wanafungua dimba na makamo-bingwa Schalke 04.Mpambano huu wa kukata na shoka utaoneshwa moja kwa moja na vituo vyqa TV katika nchi 94 ulimwenguni.

David Beckham mwishoe, aliingia uwanjani jana lakini, alisdhindwa kuiokoa klabu yake ya Los Angeles Galaxy, isizabwe bao 1:0 na Chelsea.

Al Ahly mabingwa wa Afrika wameongeza jana taji jengine walipoitimua Ismailia ili kutwaa Kombe la super Cup la Misri.

Mabingwa watetezi stuttgart wana miadi leo na makamo-bingwa Schalke 04 ambao wanakiu cha miaka 50 cha kutwaa tena ubingwa.

Timu zote mbili zinateremka uwanjani bila ya baadhi ya mastadi wao mashuhuri .Stuttgart itacheza bila mshambulizi wao Mario Gomez-aliechaguliwa mchezaji bora wa dimba mwaka 2006-7.Ameumia.Pia mturuki stadi wa kiungo Yiliray Bastruek aliejiunga kutoka Hertha Berlin,pia hatakuwa uwanjani.

Schalke, ilioongoza ngazi ya ligi hadi dakika ya mwisho msimu uliopita kabla haikuteleza kwa Stuttgart,haitakuwa na Halil Altintop na mdenmark Soren Larsen pia kwa kuwa wameumia.

Kesho duru hii ya kwanza ya Bundesliga itaendelea kwa vishindo.Mabingwa mara kadhaa Bayern munich watakuwa uwanjani wakicheza na Rostock-timu ya Ujerumani, mashariki iliopanda tena daraja ya kwanza.Munich ina shaka shaka kumteremsha kesho Luca Toni-bingwa wa dunia wa Itali ingawa ameanza mazowezi.

Munich pia itabidi kucheza bila ya chipukizi wake Lukas Podolski.Bayer Leverkusen itabidi pia kuteremka uwanjani kesho dhidi ya Energie Cottbus bila ya mbosnia Sergej Barbarez na mchezaji wa taifa Paul Freier.Pia kuna shaka-shaka iwapo mchezaji wao wa kiungo Carsten Ramelow na mlinzi Lukas Sinkiewicz aliejiunga kutoka FC Cologne,wataweza nao kucheza.

Aliepata nafuu na kurudi uwanjani ingawa katika dakika ya 72 ya mchezo ni nahodha wa zamani wa Uingereza-David Beckham.Hatahivyo,hakuweza kuisaidia klabu yake mpya ya Los Angeles Galaxy kufua dafu mbele ya Chelsea ya uingereza katika dimba la kirafiki.Chelsea iliizaba Galaxy kwa bao 1:0.

Mabingwa wa Afrika Al Ahly ya Misri ,jana waliongeza taji jengine walipoipiga kumbo kwa changamoto za mikwaju ya penalty mahasimu wao wa nyumbani Ismaili na kutwaa kombe la Super cup.

Al Ahly tayari ni mabingwa wa Misri,wa kombe la shirikisho la dimba na hapo Februari mwaka huu wakatwaa pia kombe la super cup la Afrika.jana ilikua zamu ya kombe la super cup la Misri.

Nje ya chaki ya uwanja wa dimba na Beijing ikikamilisha shamra shamra za mwaka kabla kuanza michezo ya olimpik ya majira ya kiangazi,mamia ya waumini wa madhehebu ya Falun Gong wameanzisha safari ya mwenge mjini Athens, kitovu cha miichezo ya olimpik wakidai michezo ya Beijing isusiwe kwa kuwa China inakanyaga haki za mwanadamu.

Wasichana 4 waliwasha mwenge ukiwakilisha -uhuru amani na haki katika uwanja wa Syntagma, kituo cha michezo ya awali kabisa ya Olimpik ya kisasa,1896.

Na huko China kwenyewe, wataalamu wa sayansi wanafanya majaribio ya kulisafisha anga la China na mawingu na kuizuwia mvua isifuje michezo ya Olimpik hapo mwakani.

Michezo ya 29 ya Olimpik ya majira ya kiangazi itafunguliwa August 8,2008.