1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bundesliga yaingia katika mapumziko

22 Desemba 2014

Wachezaji wa Bundesliga wana karibu wiki sita za kujiongeza nguvu upya na kuyanoa makali kwa ajili ya mzunguko wa pili wa msimu ambao utafungua pazia mnamo Januari 30. Bayern ndio mabingwa wa nusu ya msimu

https://p.dw.com/p/1E8fD
Fußball 1. Bundesliga 1. FSV Mainz 05 vs. FC Bayern München
Picha: Reuters/R. Orlowski

Mchuano utakaoanzisha shughuli hiyo ni kati ya nambari mbili Wolfsburg na viongozi Bayern Munich. Saa 22 baadaye, Borussia Bortmund kisha wataanza operesheni ya kuukokoa msimu wao ili kujiondoa katika nafasi ya pili kutoka mkiani, watakapokuwa na mchezo mgumu nyumbani kwa Bayer Leverkusen ambao wako katika nafasi ya tatu.

Bayern ambao hawajapoteza mchuano hata mmoja, wana uongozi mkubwa katika nusu ya safari ya msimu wa Bundesliga, points 11 dhidi ya mabingwa wa 2009 Wolfsburg, na kipa wa Ujerumani Manuel Neuer amefungwa mara nne pekee katika mechi 17.

Bayern wanafanya vyema hata wachezaji wao walioshinda Kombe la Dunia na wengine wa timu ya taifa hawaonyeshi dalili yoyote ya uchovu na wachezaji wapya Robert Lewandowski na Xabi Alonso wamekuwa na mwanzo mzuri sana katika mazingira mapya.

Kocha Pep Guardiola pia ameziongeza makali mbinu zake ambazo ni pamoja na kuwa na mstari wa ulinzi wenye mabeki watatu na wachezaji kutumika katika nafasi tofauti uwanjani. Aidha wana kikosi imara kilichowasaidia kujaza mapengo yaliyoachwa na wachezaji waliojeruhiwa kama vile Javi Martinez, Thiago, Bastian Schweinsteiger na nahodha Philipp Lahm.

Freiburg, wanashikilia mkia wakiwa na points 15 sawa na Borussia Dortmund, japokuwa wanapungukiwa na goli moja dhidi ya mabingwa hao wa mwaka wa 2011 na 2012. Werder Bremen, VfB Stuttgart na SV Hamburg wana points 17 kila mmoja, Hertha Berlin na Mainz 18 kila mmoja na Cologne na Paderborn wana 19 kila mmoja, na hiyo ina maana kutakuwa na kinyang'anyiro kikali cha kujiondoa katika eneo hilo la mkia ligi itakaporejea mwakani.

Mwandishi. Bruce Amani/AFP/DPA/AP/Reuters
Mhariri. Gakuba Daniel