1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bundesliga yapambamoto :

Ramadhan Ali11 Mei 2007

Klabu 3 zinaania taji -Schalke,Stuttgart na bremen kila moja yaweza kutoroka na kombe ikishinda leo na jumamosi ijayo.

https://p.dw.com/p/CHcD

Macho ya mashabiki wa dimba Ujerumani, yanakodolewa jioni hii katika viwanja vitatu vya Bundesliga-kujua iwapo kuna yeyote kati ya timu 3 za usoni zinazoweza kutwaa ubingwa itateleza jumamosi hii-Schalke inayoongoza kwa pointi moja-Stuttgart ilio nyuma kwa pointi 1 na Bremen ilionafasi ya tatu na pointi 2 tu nyuma ya Schalke huku mpambano wa mwisho jumamosi ijayo, ukitazamiwa kumtawaza bingwa kati yao.

Schalke, inaumana wakati huu na Borussia Dortmund huko Dortmund wakati Stuttgart, inacheza pia ugenini nyumbani mwa Bochum.

Bremen ni pekee kati ya timu hizo 3 za usoni inayocheza nyumbani ikichuana na Eintracht Frankfurt.

Kabla ya timu hizi kuingia hivi punde uwanjani nilizungumza na mchambuzi wetu Sekione Kitojo juu ya changamoto za leo:

Tukiacha Bundesliga inafuka moto wakati huu,huko Uingereza, Manchester United ilipanga kesho kulitembeza kombe lake la ubingwa ililolitwaa tayari mwishoni mwa wiki iliopita huko Old Trafford.Hatahivyo,kocha wao sir Alex Ferguson ,alisisitiza kwamba Manchester haitaregeza kesho kamba mbele ya West Ham licha ya kuwa taji tayari wamelitia mfukoni.

Nchini Ufaransa,Olympique Marseille, wanaingia uwanjani Stade de France mjini Paris jumamosi hii katika finali ya Kombe la taifa la Ufaransa kati yake na Sochaux.Licha ya kwamba Marseille haikuvaa taji tangu kupita miaka 14,Marseille klabu ya zamani ya Abedi Pele ilipotwaa kombe la Ulaya, ina rekodi nzuri kuliko timu yoyote ya Ufaransa katika kombe hili.

Huko Spain, viongozi wa Ligi FC Barcelona ,wanatumai jumapili kuwa historia itajirudia watakapoumana na Real Betis.Msimu uliopita, Barcelona ilikumbana pia na Real Betis lakini nyumbani mwao Barcelona walipokuwa pia kileleni mwa la Liga-ligi ya Spain sawa na ilivyo hivi sasa.Kwahivyo, mramba asali-harambi mara moja.Msimu uliopita,Barcelona iliizaba Real Betis mabao 5-1 na haikutupa tena macho nyuma na ikiwa kesho itatamba tena,Barcelona ikicheza na Ronaldinho na Samuel Eto’o itaitia tena munda Real Madrid na kutoroka kwa mara ya tatu mfululizo na taji la Spain.

Wachezaji walimtimua rifu nje ya uwanja badala ya yeye kama kawaida kuwatimua wachezaji wanaocheza ngware.Rifu Carlos Eugenio Simon aliechezesha katika Kombe la dunia mwaka jana hapa Ujerumani,aliondolewa na kikosi cha polisi nje ya Maracana Stadium baada ya ushindi wa Botafogo wa mabao 2:1 dhidi ya Atletico Miniero katika robo-finali ya Copa Brasil.Kisa ni nini ?

Rifu Simon alitoa mkwaju wa penalty dhidi ya Atletico katika muda wa kufidia.Botafogo ilisonga mbele kwa jumla ya mabao 4-3.Mara tu firimbi ya mwisho kulia, wachezaji wa Atletico walimuandama rifu Simon nay eye akafyatuka mbio.Wakaanza kumtukana na polisi hapo ikabidi kumuokoa na kutoka nae nje ya Maracana Stadium-Mecca ya dimba la Brazil.