1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bundesliga:Dortmund haikamatiki

29 Novemba 2010

Katika ligi ya Ujerumani, Bundesliga, Borussia Dortmund iliendeleza wimbi lake la ushindi pale ilipoishindilia Borussia Moenchengladbach mabao 4-1

https://p.dw.com/p/QLB6
Neven Subotic kushoto na Mats Hummels wa Dortmund wakishangilia ushindiPicha: dapd

Ushindi huo ni wa 12 kwa Dortmund katika mechi 14 na kupanua zaidi mwanya wa uongozi, ikiwa kileleni kwa pointi saba zaidi ya Mainz inayoshikilia nafasi ya pili ikiwa na pointi 30. Dortmund ina pointi 37.

Moenchengladbach ndiyo walikuwa wa kwanza kufunga, lakini Dortmund iliwabidi kusubiri hadi dakika moja kabla ya mapumziko kupachika mawili. Na kocha wake, Jürgen Kloop, alisema ni kawaida yao kutokata tamaa mpaka kipyenga cha kumaliza mpambano.

Fußball 1. Bundesliga 14. Spieltag 1. FC Kaiserslautern FC Schalke 04 Felix Magath
Felix Magath kocha wa SchalkePicha: dapd

Ama kwa upande wao wa Schalke 04, ilikuwa wiki mbaya sana kwao, pale ilipopata kipigo cha paka mwizi kwa kukandikwa mabao 5-0 na timu inayokamata nafasi ya nne kutoka mkiani ya Kaiserslautern, na kuiporomosha hadi nafasi ya 13. Kocha wa Schalke, Felix Magath, aliwatupia lawama wachezaji wake kwa kiwango duni walichoonesha.

Lakini kwa upande wa Louis van Gaal alikuwa na furaha pale timu yake, mabingwa watetezi Bayern Munich walipoifyatua Eintracht Frankfurt mabao 4-1 na kuchupa hadi nafasi ya tano.

Na habari za hivi punde zinasema kuwa FC Cologne imemtupia virago meneja wake, Michael Meier, kufuatia msimu mbaya wa timu hiyo ambayo inachungulia kaburi la kushuka daraja.

Timu hiyo pia mwezi uliyopita ilimtimua kocha wake. Zvonimir Soldo, kutokana na kuyumba huko katika Bundesliga. Jana FC Cologne ililazimishwa sare ya bao 1.1 nyumbani na Wolfsburg.

Mpaka sasa, kwa upande wa wafumaniaji nyavu, Theofanis Gekas wa Frankfurt anaongoza akiwa na mabao 12, akifuatiwa na Papiss Cisse wa Freiburg aliyepiga hodi mlangoni mara 10.

Mwandishi:Aboubakary Liongo

Mhariri:Othman Miraji