1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bundesliga:FC Cologne yatamba

7 Februari 2011

Ligi ya kandanda ya Ujerumani, Bundesliga, ambayo mwishoni mwa wiki iliingia katika raundi ya 21, iliyoshuhudia mabingwa watetezi Bayern Munich wakiteleza mbele ya FC Köln kwa kuchapwa mabao 3-2

https://p.dw.com/p/10CQw
Mshambuliaji wa FC Cologne Milivoje Novakovic akipachika bao la tatu dhidi ya Bayern Munich.Picha: AP

Kipigo hicho kimeifanya Bayern dhahiri kuonekana dhahiri kutoa mkono wa kwaheri kwa uchampioni, unaoelekea kutua Dortmund.

Katika mechi hiyo iliyofanyika mjini Köln, ambayo mpaka sasa ni gumzo kubwa katika mkoa huu wa North Rhine Westphalia, Bayern Munich walikuwa wa kwanza kupachika mabao mawili kupitia kwa Mario Gomez na Hamit Altintop.

Lakini FC Köln wakicheza kama nyati aliyejeruhiwa walicharuka, na kusawazisha mabao hayo kabla ya kupachika la tatu, kupitia kwa Christian Clemens na Milivoje Novakovic aliyepiga hodi mara mbili katika mlango wa Bayern.

Ushindi huo angalau umeanza kupunguza shaka kwa FC Koln kutumbikia katika shimo la kushuka daraja kwani sasa imefikisha pointi 22 pamoja na kwamba bado imeendelea kubakia katika nafasi ya tatu kutoka mkiani.

Kocha wa timu hiyo Frank Schaefer kama walivyo washabiki alikuwa na furaha kubwa na kusema.

´´Ni lazima niseme kuwa, kila ushindi mkubwa ninaupata na timu hii ni wetu sote, kwasababu pia kuna kitu maalum, nacho ni kuchukua pointi tatu katika bundesliga.Hiyo mara zote imekuwa ni shangwe na furaha, lakini bilashaka kwa ushindi dhidi ya Bayern Munich, baada ya mchezo mkali basi ni furaha zaidi´´

Bayern kwa kipigo hicho imeporomoka kutoka nafasi ya tatu hadi ya tano.Mapema vinara wa ligi hiyo Borussia Dortmund walilazimishwa kutoka suluhu bin suluhu na Schalke 04, lakini hata hivyo imeendelea kuchimbia kileleni kwa pointi 51 pointi 12 zaidi ya Bayer Leverkusen inayokamata nafasi ya pili.Leverkusen ikiwa na jogoo wake Michael Ballack ililambishwa mchanga na Nuremberg kwa kuchapwa bao 1-0.

Werder Bremen inayojaribu kumfukuza bundi kwenye paa lake msimu huu, ilibidi kusubiri hadi dakika za majeruhi kwa mshambuliaji wake Claudio Pizarro kusawazisha bao dhidi ya Mainz na kuufanya mpambano kuwa sare ya bao 1-1.Hannover 96 inayoonekana kukamia vilivyo msimu huu, ilichupa hadi katika nafasi ya nne kufuatia ushindi wake wa bao 1-0 dhidi ya Wolfsburg, huku Hoffenheim ikiichapa Kaiserslautern mabao 3-2.

Kwa upande wa wafumaniaji nyavu, Mario Gomez wa Bayern Munich anaongoza kwa kupachika mabao 16 akifuatiwa na Papiss Cisse wa Freiburg aliyepiga hodi mara 15 na kuitikiwa.

Mwandishi:Aboubakary Liongo

Mhariri:Mohammed Abdulrahman