1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Iraq lashambuliwa kwa bomu.

Omar Babu12 Aprili 2007

Mripuko mkubwa umetokea kwenye bunge la Iraq na kusababisha vifo vya watu watatu, wakiwemo wabunge wawili, na wengine kiasi kumi wamejeruhiwa. Kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha Iraq bomu hilo liliripuka ndani ya mkahawa wa bunge hilo.

https://p.dw.com/p/CB4k
Ndani ya jengo la bunge la Iraq. Mtu wa kujitoa mhanga ameripua bomu kwenye jengo hilo.
Ndani ya jengo la bunge la Iraq. Mtu wa kujitoa mhanga ameripua bomu kwenye jengo hilo.Picha: picture alliance/dpa

Bomu hilo liliripuka bungeni wakati wa chakula cha mchana kwenye eneo la Baghdad ambalo kwa kawaida huwekewa ulinzi mkali.

Tukio hilo ni thibitisho bayana jinsi usalama ulivyozorota katika eneo hilo la Baghdad ambalo ndilo lenye makao makuu ya serikali ya Iraq pamoja na balozi za mataifa ya kigeni.

Mripuko huo kwenye bunge la Iraq umetokea saa chache baada ya mtu wa kujitoa mhanga kuliripua lori kwenye daraja kuu la mto Tigris na kusababisha vifo vya watu kumi na magari kutumbukia mtoni.

Wakuu wa Marekani na Iraq walianzisha misako ya kiusalama kama miezi miwili iliyopita na wamefanikiwa kudhibiti kwa kiasi fulani visa vya watu kuuawa kwa kupigwa risasi.

Wakuu hao wameungama kwamba hawajamudu kulishughulikia vilivyo suala la mabomu ya kutegwa kwenye magari.

Kwa mara ya kwanza jana majeshi ya Marekani yalitoa madai kwamba waumini wa madhehebu ya Shia kutoka Iran wanaunga mkono makundi ya wanamgambo wa Kisunni ambayo yamekuwa yakitega mabomu ya magari yanayosababisha vifo vya raia pamoja na wanajeshi.

Sehemu kubwa ya daraja la Al-Sarafiyah ambalo ndilo la zamani zaidi nchini Iraq, iliporomoka kutokana na mripuko huo wa mapema leo.

Polisi wa kushika doria kwenye mto walijitahidi kutafuta watu walionusurika katika mto huo.

Afisa wa usalama alisema watu kumi walifariki na wengine ishirini na sita wakajeruhiwa.

Maafisa wengine wawili wa usalama walisema magari manne yalitumbukia mtoni kwenye daraja hilo linalounganisha mtaa wa kishia wa Al-Atafiyah katika ukingo wa magharibi wa mto Tigris na wilaya ya Kisunni ya Waziria iliyopo katika ukingo wa mashariki wa mto huo.

Wakati huo huo, Marekani imelaani waliohusika na mripuko wa bomu katika bunge la Iraq.

Hata hivyo, Marekani imeshikilia kwamba tukio hilo haliashirii udhaifu wa vikosi inavyoviongoza Marekani kufanya misako ya kiusalama mjini Baghdad.

Msemaji wa Usalama wa kitaifa wa Marekani, Gordon Johndroe, amesema mripuko huo umesababisha vifo vya watu watatu wakiwemo wabunge wawili.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Bi Condoleezza Rice ameuelezea mripuko huo kuwa njama za magaidi kutatiza jitihada mpya za kiusalama za Marekani nchini Iraq.

Bi Rice amesema:

"Bila shaka kwa mara nyingine tena hii ni kazi ya magaidi na watu wengine ambao wamedhamiria kuwazuia watu wa Iraq kuwa na mustakabali mwema wa kidemokrasia na uthabiti. Nimezingatia sana hoja kwamba jengo la bunge ndilo lililshambuliwa. Kwangu mimi shambulio la jengo ni sawa na kuishambulia taasisi yenyewe maanake bunge"

Bi Condoleezza Rice alikuwa akizungumza mjini Washington punde baada ya kushauriana na mgombea nafasi ya kuwania urais wa chama cha Republican, Seneta John McCain, ambaye ni muungaji mkono mkubwa wa sera za serikali ya Marekani nchini Iraq.

Mjini London, Waziri wa Mambo ya nje wa Uingereza, Bi Margaret Beckett ameelezea kufadhaishwa kwake na mripuko huo uliotokea katika jengo la bunge la Iraq.

Bi Margaret Beckett amewalaani waliohusika na kitendo hicho alichosema kilikuwa shambulio kwa wabunge waliochagulia kidemokrasia waliokuwa wakiendelea na shughuli zao za kila siku.