1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la shirikisho Bundestag launga mkono kutumwa Tornados nchini Afghanistan

Oummilkheir9 Machi 2007

Madege sita hadi manane ya kijeshi ya Ujerumani-Tornados yatapelekwa Afghanistan kupeleleza wapi wamejificha taliban

https://p.dw.com/p/CHIX
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Franz Josef Jung
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Franz Josef JungPicha: AP

Bunge la shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani-Bundestag,limeidhinisha kwa wingi mkubwa,mpango wa kutumwa madege ya kivita chapa Tornado nchini Afghanistan.Uamuzi huo umepitishwa katika wakati ambapo asili mia 69 ya wajerumani wanaupinga mpango huo.

Wabunge 405 kati ya 573 wameunga mkono mpango wa serikali kuu ya Ujerumani wa kutuma madege ya kijeshi chapa Tornados nchini Afghanistan.Wabunge 157 wamepinga na 11 hawakuelemea upande wowote.Kwa kupitisha uamuzi huo serikali kuu ya Ujerumani na bunge la shirikisho-Bundestag wameitika maombi ya jumuia ya kujihami ya magharibi NATO.

Madege kati ya sita na manane aina ya RECCE yatatumika kwaajili ya kukusanya habari katika maeneo ya mizozo kusini mwa Afghanistan.Marubani wa ndege hizo watakua na jukumu la kuchunguza wapi wamejificha wanamgambo wa Taliban.Tornados za Ujerumani zinasifiwa kua na teknolojia ya hali ya juu ya upelelezi kupita ndege zote za kijeshi za nchi wanachama wa jumuia ya kujihami ya Magharibi-NATO.

Wakosoaji wa mpango huo wanahoji kutumwa Tornados nchini Afghanistan ni sawa na kushiriki Ujerumani katika opereshini za kivita nchini humo.

Wanaoutetea mpango huo wanasisitiza madege hayo chapa Tornados yatachangia kuwalinda wanajeshi wa kigeni na kuwaepushia balaa la kuhujumiwa wananchi wa kawaida nchini Afghanistan.

Waziri wa ulinzi wa serikali kuu ya Ujerumani Franz Josef Jung anasema:

„Cha muhimu hapa ni kuondowa walakini ulioko katika shughuli za kukusanya habari kote nchini Afghanistan.Ni kwa masilahi ya wanajeshi wetu pia sawa na wanajeshi wa kimataifa wanaoongozwa na NATO,ISAF,wataalam wanaosimamia ujenzi mpya wa Afghanistan na raia wa kawaida pia.“

Mbali na madege hayo chapa Tornados,Ujerumani itatuma wanajeshi 500 wa ziada,watakaowekwa Mazari Sharif-kaskazini mwa Afghanistan.

Kwa mujibu wa waziri wa ulinzi Franz Josef Jung tume hii mpya ya Ujerumani itawasili Afghanistan kati kati ya mwezi ujao wa April na kusalia kwanza kwa miezi sita.

Mjadala wa bunge kuhusu kutumwa Tornados umegubikwa na kuuliwa hapo jana Dieter Rübling aliyekua akitumikia shirika la misaada ya maendeleo la Ujerumani-Welthungerhilfe kaskazini mwa nchini Afghanistan.

Wakati huo huo utafiti wa maoni ya umma umeonyesha asili mia 69 ya wajerumani wanapinga kutumwa madege hayo ya Tornados,dhidi ya asili mia 27 wanaounga mkono mpango huo.