1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Ujerumani lapiga kura kuhusu Ugiriki

27 Februari 2012

Mgogoro wa fedha wa Ugiriki,na hali nchini Afghanistan ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa zaidi na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

https://p.dw.com/p/14Abq
Jengo la bunge la shirikisho mjini BerlinPicha: picture-alliance/ ZB

Tuanzie lakini na mgogoro wa fedha wa Ugiriki.Katika wakati ambapo bunge la shirikisho-Bundestag linajiandaa kupigia kura fungu la pili la msaada wa Euro bilioni 130 kwa Ugiriki,waziri wa mambo ya ndani wa serikali kuu ya Ujerumani,Hans-Peter Friedrich anaishauri Ugiriki ijitoe katika zoni ya Euro.Gazeti la "Nordbayerischer Kurier" linaandika:Hans Peter Friedrich amejitenganisha na msimamo wa kansela na pia wa mwenyekiti wa chama chake mwenyewe .Mwanasiasa huyo wa kutoka chama cha CSU amekuwa waziri wa kwanza wa serikali kuu ya Ujerumani kuisihi Ugiriki iachane na sarafu ya Euro.Yadhihirika kana kwamba kuna wabunge wengi zaidi miongoni mwa wafuasi wa vyama ndugu vya CDU/CSU na waliberali wa FDP kuliko vile ilivyofikiriwa wanaopanga kuupinga msaada ziada wa fedha kwa Ugiriki.Hofu ya kisasi cha wapiga kura ndio inayaowafanya wafuate msimamo huo.

Bundesinnenminister Hans-Peter Friedrich zur Neonazi-Verbunddatei
Waziri wa mambo ya ndani Hans-Peter FriedrichPicha: dapd

Licha ya mwito wa waziri wa mambo ya ndani,gazeti la "Neue Osnabrücker Zeitung" linahisi mpango wa kuipatia Ugiriki fungu la pili la msaada wa fedha,utaungwa mkono na wengi bungeni.Gazeti linaendelea kuandika:Shauri la waziri wa ndani wa serikali kuu Hans Peter Friedrich kwa viongozi wa serikali mjini Athens halifuatani kabisa na msimamo wa serikali ya Berlin inayoitaka Ugiriki isalie katika umoja wa sarafu.Shauri hilo haliashirii mema kwa kura ya leo bungeni.Ingawa wingi unaohitajika utapatikana.Hata hivyo lakini kimoja ni dhahir pia nacho ni kwamba itakuwa shida kukusanya misaada ziada kwa washirika watakaokuwa na dhiki siku za mbele.Ikiwa wanachama wa serikali hawana msimamo mmoja,usishangae kwa hivyo ukisikia kama idadi ya wenye wasiwasi inazidi kuongezeka miongoni mwa wabunge.

Gazeti la "Sächsische Zeitung" linaandika:Hans Peter Friedrich ni miongoni mwa wale wanaozidi kuongezeka katika serikali ya muungano,wanaohisi,hata fungu hili la pili la msaada halitotosha .Pengine hawajakosea.Lakini kujitoa Ugiriki katika kanda ya Euro kutasababisha hasara kubwa zaidi kwa Ujerumani na walipa kodi wake kuliko kutoa fungu la tatu au la nne la misaada.

Griechenland Parlament Athen Proteste
Maandamano mbele ya bunge la UgirikiPicha: REUTERS

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu hali namna ilivyo nchini Afghanistan.Gazeti la "Kieler Nachrichten" linaandika:Afghanistan haitaweza kujipatia mfumo wa vyama vingi na wa kidemokrasia mnamo muda mfupi ujao.Huo ndio mtazamo uliojitokeza baada ya juhudi za mwongo mzima kushindwa kuleta tija.Nchi za magharibi zimeshindwa nchini Afghanistan.Hatari ni kubwa kuiona Afghanistan,sawa na Pakistan ikigeuka tena kuwa mahala wanakojificha magaidi wa kiislam.Hatari kubwa zaidi lakini ni kuona watu wakipoteza imani walio nayo:Kuna faida gani ya kuyatia hatarini maisha ya wanajeshi kupigania kituo ambacho tokea hapo hakina nafasi ya kufanikiwa."

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Abdul-Rahman, Mohammed