1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge lamkingia kifua Temer

Lilian Mtono
14 Julai 2017

Kamati ya bunge la Brazil jana imepiga kura kupinga hatua ya kuwasilishwa kesi ya madai ya rushwa yanayomkabili Rais wa nchi hiyo Michel Temer kufikishwa mahakama ya juu zaidi ili kiongozi huyo afunguliwe mashtaka.

https://p.dw.com/p/2gWfr
Brasilien Michel Temer
Picha: Agência Brasil/Valter Campanato

Kura hiyo haina nguvu kisheria, na bunge zima litazimika kupiga kura dhidi ya madai hayo, ambayo yanaweza kuidhinishwa iwapo tu theluthi mbili ya wabunge watapiga kura hiyo. Temer alishitakiwa mwezi uliopita akihusishwa na njama za matumizi mabaya ya fedha za umma, yanayohusisha kampuni kubwa duniani ya kusindika nyama, JBS. 

Mwendesha mashtaka mkuu Rodrigo Janot alimtuhumu Temer kwa kuratibu mpango wa kupokea rushwa ya kiasi cha Dola Milioni 11.85 kutoka JBS, katika miezi tisa inayokuja

Bunge zima litapiga kura Agosti 2, ikiwa ni baada ya wiki mbili za mapumziko. Ingawa uungaji mkono wa Temer unapungua, lakini bado anaamini kwa kiasi kikubwa kushinda kishindo hicho cha kura ya bunge zima.

Hata hivyo, mwendesha mashtaka, Janot alisema anatarajia kuwasilisha mashtaka mawili mapya ya wizi wa mali ya umma dhidi ya Temer katika kipindi cha wiki chache zijazo. 

Brasilien Abgeordnetenhaus
Baadhi ya wabunge wanasema kama wangepiga kura mara kadhaa, kungekuwa na uwezekano wa moja ya mshtaka kukubaliwa bungeni Picha: Agência Brasil/Wilson Dias

Baadhi ya wabunge wameliambia shirika la habari la Reuters katika wiki za hivi karibuni kwamba kama wangelazimishwa kupiga kura kwa mara kadhaa ili kumlinda kiongozi huyo aliyepungua umaarufu dhidi ya kufunguliwa mashtaka, uwezekano wa moja ya mashtaka hayo kukubaliwa na bunge utaongezeka kwa kiasi kikubwa.

Hapo jana, Rais Temer alinukuliwa akisema anaangalia namna ya kuirejesha Brazil kwenye njia sahihi, ingawa kamati hiyo ya bunge ilikuwa ikijiandaa kupiga kura ya kufungua mashtaka ya rushwa dhidi yake.

Hatua hiyo ya kamati ya bunge inachukuliwa kama ishara ya ushindi kwa Temer ikiwa ni siku moja baada ya rais ya zamani Lula da Silva kuhukumiwa kifungo cha miaka 9 kwa mashitaka ya matumizi mabaya ya mali ya umma. 

Kesi za rushwa dhidi ya viongozi hao wakubwa wawili nchini Brazil zinathibitisha kiwango cha mzozo wa kisiasa katika taifa hilo kubwa zaidi katika bara la Latin Amerika, ambako uchunguzi mpana wa rushwa umefichua mipango ya rushwa na malipo ya shukrani yasiyo halali kwa ajili ya upendelo wa kisiasa na mikataba ya umma. Hata hivyo Temer anakataa madai hayo dhidi yake.     

Temer alichukua nafasi hiyo baada ya kuenguliwa kwa Dilma Rouseff kufuatia madai kama hayo ya matumizi mabaya ya fedha za umma mwaka jana, ataweza kuondolewa ndani ya angalau siku 180 iwapo angelazimika kusimama mbele ya mahakama hiyo ya juu zaidi.

Mwandishi: Lilian Mtono./Afpe/Ape/Rtre
Mhariri: Gakuba, Daniel