1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Buriani "chui mweusi" Eusebio

6 Januari 2014

Buriani Chui mweusi , Eusebio da Silva Ferreira, wapenzi wa soka duniani kote wamlilia mchezaji huyo nyota mzaliwa wa Msumbiji aliyefariki jana Jumapili(05.01.2014) nchini Ureno.

https://p.dw.com/p/1AlzT
Portugals Fußball-Legende Eusebio ist tot
Chui Mweusi, Eusebio da Silva FerreiraPicha: picture-alliance/Pressefoto UL

Eusebio da Silva Perreira , maarufu kama Eusebio ama jina la utani "Chui mweusi", amefariki jana Jumapili akiwa na umri wa miaka 71, na kifo chake kimewaletea mashabiki wengi simanzi , wakimkumbuka nyota huyo ambaye alitokea katika bara la Afrika nchini Msumbiji na kuwa mmoja kati ya wachezaji nyota duniani.

Eusebio aliyefariki siku ya Jumapili asubuhi kutokana na moyo wake kushindwa kufanyakazi, alitawala soka nchini Ureno katika miaka ya 1960, na kuiletea sifa nchi hiyo pamoja na klabu yake ya Benfica Lisbon. Serikali ya Ureno imetangaza siku tatu za maombolezo, na bendera mjini Lisbon zinapepea nusu mlingoti kabla ya mazishi yake siku ya Jumatatu ambapo mamia kwa maelfu ya watu wanatarajiwa kujipanga mitaani kutoa heshima zao za mwisho.

Portugals Fußball-Legende Eusebio ist tot
Eusebio akiwa na Ronaldo (kulia)Picha: AFP/Getty Images

Wachezaji kadha wa zamani ikiwa ni pamoja na Bobby Chalton ambaye aliisaidia Manchester United kupata ushindi dhidi ya Benfica katika mwaka 1968 katika fainali ya kombe la Ulaya ambalo sasa ni champions League , amesema ilikuwa ni nafasi ya pekee kumfahamu Eusebio. Franz Beckenbeuer nahodha wa timu ya taifa ya Ujerumani katika kombe la dunia 1970 , 74 na 78 amemueleza Eusebio kama rafiki yake na nyota wa wakati huo.

Kwa wengi Eusebio aliyezaliwa mwaka 1942 nchini Msumbiji hadi leo hii ndie mchezaji bora kabisa katika historia ya soka nchini Ureno na mchezaji wa kwanza nyota kutoka bara la Afrika. Ameisaidia timu yake ya Benfica kupata mafanikio kadha kitaifa na kimataifa. Mwandishi wa habari za michezo mzaliwa wa Msumbiji Jose Musuaili alimpenda sana Eusebio tangu akiwa mtoto , licha ya kuwa yeye binafsi alikuwa shabiki mkubwa wa timu hasimu nchini Ureno ya Sporting Lisbon.

Bildergalerie Fußballer Eusebio
Eusebio da Silva FerreiraPicha: picture-alliance/dpa

"Alikuwa kipenzi cha kizazi chote cha baba zetu. Na hata leo ni alama maalum kwetu. Sio tu kwa wapenzi wa soka kwa sisi Waafrika, lakini pia kwa watu wote, ambao wanazungumza lugha ya Kireno. Nimebahatika, kuwa rafiki wa familia ya Eusebio. Katika mahojiano yangu ya kwanza na Eusebio , nilitambua kuwa Eusebio kwa kweli yuko kama tunavyomuona. Kwa upande mmoja ni nyota wa soka la Ureno na kimataifa, lakini kwa upande mwingine ni mtu wa kawaida kabisa."

Bildergalerie Fußballer Eusebio
Eusebio akifunga baoPicha: picture-alliance/dpa

Eusebio aliichezea Ureno mara 64 alifunga mabao 41. Pia alituzwa kiatu cha dhahabu mara mbili na amekuwa mfungaji bora nchini Ureno kati ya mwaka 1964 na 1973. Aliipatia ushindi wa ligi Benfica mara 11 pamoja na vikombe vitano vya chama cha mpira nchini Ureno. Aliistaafu soka mwaka 1979. Mungu amlaze mahali pema . Ameen.

Portugal Lissabon Trauerfeier Eusebio
Mashabiki wakimuenzi EusebioPicha: Miguel Riopa/AFP/Getty Images

Robert Lewandowsky mshambuliaji wa Borussia Dortmund ya Ujerumani anahamia kwa mahasimu wakubwa wa timu hiyo Bayern Munich msimu ujao. Lakini Lewandowsky amewatuliza jana wapenzi wa Dortmund kwa kusema " tuna nusu mwaka mbele yetu, ambapo tuna malengo maalum ambayo tunataka kuyatimiza," Licha ya kuwa kuna baadhi ya wapenzi wa Borussia ambao hawakubaliani na uamuzi wangu, nina matumaini ya kupata uungwaji mkono katika kila mchezo, nitatoa kila nilichonacho kwa BVB. amesema mshambuliaji huyo katika tovuti ya klabu.

Robert Lewandowski Fußballspieler ARCHIV 2012
Robert Lewandowsky atavalia msimu ujao jezi ya Bayern MunichPicha: picture-alliance/dpa

Wakati huo huo vilabu vinavyoshiriki ligi ya Ujerumani Bundesliga ambayo iko mapumzikoni hivi sasa vimeanza rasmi kambi ya mazowezi wiki hii. Mabingwa wa Bundesliga Bayern Munich na Schalke 04 wako nchini Dubai , makamu bingwa Borussia Dortmund wanaanza kambi nchini Uhispania wiki ijayo na Bayer Leverkusen halikadhalika wako nchini Uhispania.

Mshambuliaji wa pembeni wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ufaransa Frank Ribery wakati huo huo ameteuliwa na mchezaji bora wa katika nusu ya kwanza ya ligi ya Ujerumani Bundesliga na wachezaji wenzake wa ligi hiyo. Arjen Robben pia wa Bayern ameshika nafasi ya pili wakati Marco Reus wa Borussia Dortmund ameshika nafasi ya tatu.

UEFA Champions League Manchester City - Bayern München
Frank Ribery( kulia)Picha: Reuters

Ligi za mataifa mengine hata hivyo zinaendelea , ambapo hapo jana Juventus Turin ilitunisha misuli yake dhidi ya Roma na kuirarua kwa mabao 3-0. Kabla ya hapo Fiorentina iliibuka kidedea kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Livorno.

Wakati huo huo matumaini ya mshambuliaji wa Italia Giuseppe Rossi kucheza katika kombe la dunia huenda yakatatizwa baada ya mchezaji huyo wa Fiorentina kupata maumivu katika goti lake la mguu wa kulia ambalo limekuwa na matatizo kila mara katika mchezo wa jana Jumapili dhidi ya Livorno.

Wakati huo huo Gareth Bale amepona maumivu katika mguu wake wa kushoto na atakuwamo katika kikosi cha Real Madrid ambacho kitashuka dimbani leo jioni kupambana na Celta Vigo.

Katika michezo ya jana Jumapili katika ligi ya Uhispania la Liga Barcelona iliirarua Elche kwa kuipa kipigo cha mabao 4-0. Ushindi huo wa Barca hata hivyo umekuja bila ya mshambuliaji wake hatari Lionel Messi.

Kocha wa Barcelona Gerardo Tata Martino amesisitiza hata hivyo kuwa hatamharakisha Messi kurejea dimbani katika pambano la wababe walioko kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo dhidi ya Atletico Madrid mwishoni mwa juma lijalo. Messi hajacheza tangu alipoumia misuli katika mchezo dhidi ya Real Betis mapema mwezi Nivemba na alikuwa mtazamaji tu wakati mabingwa hao waliporejea kileleni mwa msimamo wa ligi jana katika ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Elche.

Manchester United itaangalia majaliwa yake katika kombe la ligi ili kurejesha imani kwa mashabiki katika msimu huu wakati watakapokuwa wageni wa Sunderland kesho Jumanne katika mchezo wa kwanza katika nusu fainali.

Jana Jumapili Manchester United iliangukia pua pale ilipoyaaga mashindano ya mwaka huu ya kombe la FA baada ya kuzabwa mabao 2-1 dhidi ya Swansea City katika uwanja wa nyumbani wa Theather of Dreams , Old Trafford.

Licha ya kuwa United bado inaendelea kucheza katika harusi mbili , ligi ya mabingwa wa Ulaya Champions League na kombe la ligi, kombe hilo ndio matumaini yao makubwa kuweza kuokoa msimu ambao unaonekana kuwa wa maafa.

FC Everton Trainer David Moyes
David Moyes kocha wa Manchester UnitedPicha: Getty Images

Wakati kocha wa zamani wa Manchester United Sir Alex Ferguson hatimaye alipobwaga manyanga katika kazi ya kuifunza timu hiyo alisimama katika nyasi za Old Trafford na kuwatafadhalisha mashabiki wa Man United kumpa ushirikiano na kumuunga mkono mrithi wake aliyemteua David Moyes kwa kukumbuka nyakati mbaya pamoja na zile nzuri.

Lakini baada ya jana Manchester United kunyofolewa kutoka katika kinyang'anyiro hicho cha kombe la FA mashabiki hawakusita kuonesha kufadhaika kwao.

Chelsea wamepangwa dhidi ya Stoke City katika kombe hilo la FA katika duru ya nne katika upangaji wa mchezo hiyo jana Jumapili. Liverpool ambayo iliiangusha Oldham Athletic kwa mabao 2-0 jana itawatembelea Bournermouth ama Burton Albion. Zawadi ya Swasea City kwa kuwaondoa Manchester United katika kinyang'anyiro hicho itakuwa ziara kwa Birmingham City , Bristol Rovers ama Crawley Town.

Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe / rtre / ape

Mhariri : Mohammed Abdul Rahman