1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utawala wa kiraia kurejeshwa Burkina Faso

20 Septemba 2015

Burkina Faso itairejesha madarakani serikali ya mpito inayoongozwa na Rais Michel Kafando katika kile kitakachokuwa ni ushindi kwa waandamanaji dhidi ya viongozi wa mapinduzi.

https://p.dw.com/p/1GZFq
Burkina Faso Ouagadougou General Gilbert Diendere
Kiongozi wa mapinduzi jenerali Gilbert DienderePicha: Getty Images/AFP/S. Kambou

Rais Thomas Boni Yayi wa Benin, ambaye anaongoza wapatanishi wa mataifa ya Afrika, alisema hapo Jumamosi (19 Septemba) kwamba wana matumaini tena ya kurejea madarakani kwa Kafando.

Baada ya duru ya tatu ya mazungumzo na kiongozi wa mapinduzi hayo, Jenerali Gilbert Diendere, Rais Yayi aliwaambia waandishi wa habari mjini Ougadougou kwamba: "Tutazindua kipindi cha mpito ambacho kilikuwa kinaendelea - kipindi cha mpito kilichokuwa kinaendeshwa na raia, pamoja na Michel Kafando," akiongeza kuwa taarifa zaidi za "habari hizo nzuri" zingetolewa Jumapili.

Burkina Faso Protest gegen den Putsch in Ouagadougou
Waandamanaji wakipinga jeshi kutwaa madaraka Burkina FasoPicha: Reuters/J. Penney

Wataka kuzuwia ghasia

Wakitaka kufikisha mwisho mapambano ya ghasia baina ya wanajeshi na waandamanaji na kuwezesha kufanyika kwa uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika mwezi Oktoba, wapatanishi wa kutoka bara la Afrika walifanya mazungumzo na Jenerali Diendere.

Rais wa Senegal Macky Sall, ambaye pia anapatanisha katika mzozo huo kama mkuu wa mataifa ya eneo hilo ECOWAS, hakutoa maelezo yoyote baada ya mazungumzo hayo.

Ofisi yake hapo kabla ilithibitisha kuwa anatafuta kupatanisha kurejea madarakani kwa Kafando.

Burkina Faso Protest gegen den Putsch in Ouagadougou
Waandamanaji mitaani mjini OuagadougouPicha: Reuters/J. Penney

Haikufahamika wazi iwapo madai hayo ya makubaliano yanahusisha msamaha kwa Diendere, jenerali kivuli ambaye alitumika kama mkuu wa usalama wa taifa chini ya rais aliyeondolewa madarakani Blaise Compaore.

Pia haijakuwa wazi iwapo utaratibu wa uchaguzi utaweza kurejeshwa.

Wanajeshi wana wasi wasi kufutwa kwa kikosi chao

Diendere hakukana kwamba makubaliano ya awali yamefikiwa. "Kila mara nimesema kwamba sitang'ang'ania madarakani. Sasa ni suala la masharti," amewaambia waandishi habari baada ya mkutano.

Wanajeshi kutoka katika kikosi cha ulinzi wa rais walivamia mkutano wa baraza la mawaziri siku ya Jumatano na kumkamata rais Kafando na mawaziri, wakivuruga utaratibu wa kipindi cha mpito ambacho kilitarajiwa kumalizika kwa uchaguzi wa rais Oktoba 11.

Burkina Faso Protest gegen die Präsidentengarde in Ouagadougou
Maandamano ya kupinga mapinduzi Burkina FasoPicha: Reuters/J. Penney

Wakijiita baraza la taifa la demokrasia, viongozi wa mapinduzi wanapinga mipango ya serikali ya mpito kuvunja kikosi cha ulinzi wa rais na kudai nchi hiyo inakabiliwa na hali ya kutokuwa thabiti baad ya baadhi ya wagombea kuzuiwa kugombea katika uchaguzi huo.

"Tunataka tu kwamba baadhi ya mapendekezo ambayo yataturuhusu kuingia katika uchaguzi kwa amani na utulivu wakati kutahakikishwa kwamba matokeo hayatapingwa na hayawezi kupingwa," Diendere amekiambia kituo cha televisheni cha TV 5 mapema jana.

Umoja wa Afrika watoa muda maalum

Umoja wa Afrika umesitisha uanachama wa taifa hilo la Afrika magharibi na kuwapa viongozi hao wa mapinduzi masaa 96, ama hadi Septemba 22, kurejesha serikali ya zamani.

Mapinduzi hayo yameshutumiwa pia na Marekani, Ufaransa ambayo ni mkoloni wa zamani na Umoja wa mataifa.

Burkina Faso Protest gegen die Präsidentengarde in Ouagadougou
Waandamanaji wakiingia mitaani kupinga mapinduzi Burkina FasoPicha: Reuters/J. Penney

Chini ya Compaore, Burkina Faso ilijitokeza kuwa mshirika mkubwa wa Ufaransa na Marekani katika eneo hilo dhidi ya wanamgambo wenye mafungamano na al-Qaeda ambao wanafikiriwa wanaendesha harakati zao katika eneo la kaskazini pamoja na nchi jirani ya Mali.

Mwandishi: Sekione Kitojo/rtre

Mhariri: Mohammed Khelef