1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Burkina Faso na Gabon zafunga virago

26 Januari 2015

Mzunguko wa mwisho wa duru ya makundi katika kombe la mataifa ya Afrika wazusha mshangao, Gabon na Burkina Faso zilizopigiwa upatu kuingia robo fainali zafungasha virago kutoka Guinea ya Ikweta.

https://p.dw.com/p/1EQiM
Kongo gegen Burkina Faso African Cup of Nations 2015
Wachezaji wa Guinea ya Ikweta wakisherehekea ushindi dhidi ya GabonPicha: K.Desouki/AFP/Getty Images

Wenyeji wa mashindano ya fainali za kombe la mataifa ya Afrika Guinea ya Ikweta wanaelekeza sasa macho yao kuweza kupata mafanikio makubwa zaidi baada ya sherehe kubwa kupokea ushindi jana jioni na kufuzu kuingia katika duru ya robo fainali.

Kikosi cha timu ya taifa ya Guinea ya Ikweta kijulikanacho kama Taifa Nzalang kiliishinda Gabon katika mchezo wao wa mwisho katika kundi A mjini Bata na kufanikiwa kusonga mbele kwa ushindi wa mabao 2-0.

Gabun gegen Äuatorialguinea African Cup of Nations 2015
Furaha isiyo kifani kwa Guinea ya Ikweta kuingia robo fainaliPicha: C.de Souza/AFP/Getty Images

Wanashika nafasi ya pili katika kundi hilo nyuma ya Congo Brazzaville wakiwa na pointi tano na sasa wanaweza kuweka matumaini yao katika mpambano wa robo fainali na mshindi wa kundi B mjini Ebebiyin siku ya Jumamosi.

"Tunafikiri tu kuhusu mchezo ujao na tunaimani tutajitahidi bila kujadili ni timu gani tutapambana nayo," amesema Balboa, mchezaji ambaye amepitia mafunzo katika timu za vijana za Real Madrid nchini Uhispania ambaye hivi sasa anacheza soka nchini Ureno.

Miaka mitatu iliyopita , Guinea ya Ikweta pia ilifikia robo fainali kama wenyeji wenza pamoja na Gabon , lakini hatimaye walisalim amri dhidi ya Cote D'Ivoire kwa mabao 3-0.

Umoja katika kikosi cha Guinea ya Ikweta

Wakati huo Nzalang Nacional iliundwa na wachezaji waliopata urai wakitokea nchi kama Brazil na Colombia. Lakini mashabiki na wachezaji kwa pamoja hivi sasa wanazungumza kwa fahari zaidi kuhusu kikosi hiki, wakieleza kwamba wachezaji wote 23 wa kikosi hicho wana mizizi yao halisi katika nchi hiyo ndogo ya Afrika ya kati.

Burkina Faso Fußball Nationalmannschaft
Timu ya taifa ya Burkina Faso inayorejea nyumbaniPicha: B. Stansall/AFP/Getty Images

"Nguvu yetu kwa sasa ni kwamba timu yetu ina umoja. Mwaka 2012 , tulikuwa na wachezaji wengi ambao hawakuwa wanatoka nchini humu na mashabiki hawakuwa wakifurahia hilo na hawakuwa na fahari kama walivyo hivi sasa juu ya timu yao ya taifa, " mchezaji wa kati mzaliwa wa Uhispania Juvenal Edjogo-Owono amesema.

Katikakti ya mwaka jana Guinea ya Ikweta iliondolewa mashindanoni kutokana na kumchezesha mchezaji ambaye hakustahili kucheza dhidi ya Mauritania , na walirejeshwa tu kama wenyeji baada ya Morocco kujitoa kutokana na hofu ya ugonjwa wa Ebola.

Uamuzi huo wa dakika za mwisho na kuteuliwa kwa kocha mpya kutoka Argentina Esteban Becker mwanzoni mwa mwezi huu, kuliwaweka katika hali ya kutokuwa na muda mzuri wa matayarisho kwa fainali hizo.

Leo hii kundi B linamaliza michezo yake ambapo Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo ina miadi na Tunisia wakati huo huo nyasi zitawaka moto mjini Ebebiyin wakati Cape Verde itakapotiana kifuani na Zambia mabingwa wa mwaka 2012 wa kombe la mataifa ya Afrika.

Kongo Fußball Nationalmannschaft
Kikosi cha timu ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya CongoPicha: I. Sanogo/AFP/GettyImages

Tunisia inaongoza katika kundi hilo baada ya kupata pointi 4 , ikitoka sare na Cape Verde na kuishinda Zambia kwa bao 1-0 , ikifuatiwa na Cape Verde na Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo na ya mwisho Zambia ikiwa na pointi moja. mambo hata hivyo yanaweza kubadilika iwapo Zambia chipolopolo watashinda dhidi ya Cape Verde na Tunisia ikiishinda Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo.

Kesho ni zamu ya kundi C, ambapo kundi hilo linaloangaliwa kama kundi gumu kabisa katika mashindano haya lina timu za Algeria, Senegal , Ghana na Afrika kusini. Bado kundi hili ni gumu kwa kuwa baada ya mzunguko wa michezo miwili , Senegal inaongoza kundi hilo kwa kuwa na pointi 4, ikifuatiwa na Algeria yenye pointi 3 , Ghana pia ina pointi 3 na mwishoni iko Afrika kusini yenye pointi 1.

Lakini mambo yanaweza kubadilika iwapo Senegal itafungwa na Algeria, na Afrika kusini ikaifunga Ghana katika mchezo wao wa mwisho kesho Jumanne.

Africa Cup of Nations 2014 - Senegal vs. Ägypten
Wachezaji wa SenegalPicha: Khaled Desouki/AFP/Getty Images

Kila kitu kinawezekana wakati viongozi wa kundi hilo Senegal wanapambana na Ageria iliyokuwa ikipigiwa upatu kutoroka na kombe hilo mwanzoni mwa mashindano haya mjini Malabo wakati Ghana inatiana kifuani na Afrika kusini mjini Mongomo.

Kuna tufauti kubwa ya mambo katika viwanja hivyo wakati timu zote vinawania kuingia katika awamu ya mtoano , licha ya kuwa kikosi cha Alain Giresse cha Simba wa Teranga , Senegal kinatambua kuwa sare inatosha kuwavusha katika awamu ya mtoano dhidi ya algeria, wakati ushindi utahakikisha nafasi yao kuingia katika robo fainali.

Hata hivyo kikosi cha Christian Gourcuff , Algeria kinaweza kuvuka kikwazo hiki na kuingia katika robo fainali pia iwapo Afrika kusini itaifunga Ghana. Wakati huo huo mjini Mongomo Ghana inaweza kuingia katika robo fainali iwapo itashinda tu, wakati sare itatosha iwapo Algeria haitashinda dhidi ya Senegal.

Bingwa wa bara la Asia

Katika bara la Asia , Korea ya kusini imeingia katika fainali ya kombe la mataifa ya Asia kwa kushinda michezo mitano bila la kufungwa bao lakini kocha Mjerumani Uli Stielike ameonya kuwa kunahitajika ubora zaidi ili kuweza kunyakua taji la mataifa ya bara hilo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1960.

Uli Stielike
Uli Stielike kocha wa Korea kusiniPicha: imago/Schüler

Ushindi wa mwisho ulikuwa wa mabao 2-0 katika nusu fainali dhidi ya Iraq ambamo timu hiyo haikuonesha dalili za kushindwa.

Australia nayo , kama timu nyingine katika kinyang'anyiro hicho , haina hakika kwamba kila kitu kinakwenda kwa mujibu ya mipango yao, hali ambayo inakifanya kikosi hicho kuwa na wasi wasi na Umoja wa falme za kiarabu wakati watakapopambana leo.

Iwapo kila kitu kingekwenda kwa mujibu wa mipango yao , wenyeji hao wa mashindano wangeingia dimbani katika uwanja wa mjini Sydney wa Olimpik , leo siku ambayo pia ni siku ya taifa hilo la Australia.

Lakini baada ya kupoteza mchezo wao dhidi ya Korea ya kusini katika mchezo wa makundi , njia ya Australia ilibadilika na sasa wanacheza mchezo wa nusu fainali mjini Newcastle, uwanja ambao una uwezo wa kuingiza kiai wa watu 20,000 tu, dhidi ya UAE, timu ambayo ilishangaza Japan mabingwa watetezi katika robo fainali.

Ligi ya Ujerumani Bundesliga

Na katika ligi ya Ujerumani Bundesliga, kazi waliyonayo makamu bingwa wa Bundesliga , Borussia Dortmund kuepuka kushuka daraja haitachafuliwa na mazungumzo ya mara kwa mara ya uhamisho unaohusishwa na wachezaji nyota wa timu hiyo , mlinzi Mats hummels amesema leo.

Deutschland Fußball Bundesliga Borussia Dortmund Mats Hummels
Mlinzi wa Borussia Dortmund Mats HummelsPicha: imago/T. Zimmermann

Dortmund , ambao pia walikuwa mabingwa wa Bundesliga katika msimu wa mwaka 2011 na 2012, wako nafasi ya 17 katika ligi, wakiwa sawa kwa pointi na Freiburg ambayo iko mkiani baada ya nusu msimu kumalizika ambapo walipoteza michezo 10 kati ya 17.

Mlinzi wa kati Mats Hummels na mshambuliaji wa pembeni Marco Reus pamoja na mchezaji wa kati Ilkay Gurndogan wanaripotiwa kumezewa mate na vilabu vikubwa barani Ulaya iwapo Borussia itashindwa kucheza katika michuano ya vikombe vya Ulaya msimu ujao hali iayozidisha uvumi.

Ligi ya Ujerumani Bundesliga inarejea uwanjani Ijumaa , katika pambano la ufunguzi kati ya mabingwa na viongozi wa ligi hiyo Bayern Munich wakiikaribisha Bayer Leverkusen.

Wakati huo huo kocha wa mabingwa hao Pep Guardiola ameonekana kutokuwa na haraka ya kutia saini makubaliano mapya ya kuifunza timu hiyo kupindukia mwaka 2016.

Fußball Champions League Gruppe E FC Bayern München Manchester City Pep Guardiola
Kocha wa Bayern Munich Pep GuardiolaPicha: picture-alliance/dpa/Sven Hoppe

Guardiola ameiongoza Bayern Munich kunyakua ubingwa wa Ujerumani na kombe la shirikisho katika msimu wa kwanza mwaka jana lakini mazungumzo ya kurefusha mkataba wake wa miaka mitatu yatafanyika baadaye mwaka huu.

Mwandishi Sekion Kitojo / dpae / ape / afpe / rtre

Mhariri: Iddi Ssessanga