1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali nchini Burundi inatia wasi wasi

13 Novemba 2015

Hali nchini Burundi na mkutano wa kilele wa Valleta Malta kati ya viongozi wa Afrika na wale wa Umoja wa ulaya ni miongoni mwa mada za Afrika zilizogonga vichwa vya habari nchini Ujerumani wiki hii.

https://p.dw.com/p/1H55H
Watu wanakimbia matumizi ya nguvu BurundiPicha: picture-alliance/AP Photo

Tuanzie na hali nchini Burundi ambako Umoja wa Ulaya unapanga kupunguza idadi ya wafanyakazi katika ofisi zake nchini humo pamoja na kuwarejesha nyumbani familia za wafanyakazi wa kigeni kutokana na kitisho cha kuzuka mapigano nchini humo."Kitisho cha kuzuka mauwaji ya halaiki" ndio kichwa cha maneno cha gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linalochambua "onyo la mwisho" la serikali kwa upande wa upinzani pamoja pia na mikururo ya watu wanaoyapa kisogo maskani yao.Watu wanaomiliki silaha walipewa muda wa hadi jumapili ya wiki iliyopita kuzisalimisha silaha hizo.Onyo hilo limewalenga zaidi watu wa kabila dogo la Tutsi linaandika gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linalomnukuu rais Pierre Nkurunziza akisema katika hotuba yake kwa taifa "hili ni onyo la mwisho".Umoja wa Mataifa na wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani wanayataja matamshi hayo kuwa ni ya hatari.Frankfurter Allgemeine limemnukuu pia waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier akisema hali namna ilivyo nchini Burundi inakumbusha maovu yaliyotendeka wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe na mauwaji.

Kitisho cha kuzuka mauwaji ya halaiki nchini Burundi kimetajwa pia na mhariri wa gazeti la mjini Berlin,die Tageszeitung.Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililokutana kwa kikao cha dharura halijui lifanye nini katika nchi hiyo inayoelekea "kuzama ". Kila kukicha mitandao ya kijamii mjini Bujumbura inazungumzia juu ya idadi ya maiti zinazogunduliwa alfajiri majiani.Mkuu wa halmashauri ya Umoja wa mataifa inayoshughulikia masuala ya haki za binaadam Zeid Ra'ad al Hussein amelitaka baraza hilo lipitishe hatua zote zinazowezekana.Kuna hofu ya kuenea mzozo wa Burundi hadi katika nchi jirani ya Rwanda ikiwa rais Pierre Nkurunziza,ambae ni wa kabila la Hutu atawalenga zaidi watu wa kabila la Tutsi ambao kwa upande wao watategemea ulinzi kutoka kwa rais wa Rwanda Paul Kagame ambae ni wa kabila la watutsi.Die Tageszeitung limezungumzia hotuba iliyotangazwa na kituo cha matangazo ya kimataifa cha Ufaransa RFI ambapo rais wa Paul Kagame ambae binafsi aliwahi wakati mmoja kukomesha mauwaji ya halaiki anasema "Wananyarwanda wanalazimika kujihami dhidi ya maovu,yasije yakarejea tena."

Mkutano wa Valletta kuhusu wakimbizi

Mada nyengine ya Afrika iliyogonga vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani wiki hii,inahusiana na mkutano wa kilele wa viongozi wa Afrika na Umoja wa Ulaya,kuhusu wakimbizi mjini Valletta nchini Malta.Magazeti yote mashuhuri,Frankfurter Allgemeiner,Berliner Zeitung,Der Tagesspiegel na kadhalika yamezungumzia mkutano huo wa kilele ulioamua kutenga kitita cha Euro bilioni mbili kuzisaidia nchi za Afrika kukabiliana na wimbi la wakimbizi.Gazeti la kusini mwa Ujerumani "Süddeutsche Zeitung" linachambua umuhimu wa mji na nchi mkutano huo wa kilele ulikoitishwa.VaIletta,mji mkuu wa kisiwa cha Malta kilichoko kati kati ya bahari ya Mediterenia eneo linaloyaunganisha mabara yote mawili Afrika na ulaya.Afrika na Ulaya wanakutana kwa hivyo kati kati kuzungumzia mzozo wa wakimbizi linaandika gazeti la Süddeutsche Zeitung.Ni ujinga kuamini kwamba viongozi wa taifa na serikali barani Afrika wana moyo wa kuzuwia wimbi la wahamiaji.Wengi wao wanaona pengine ni vyema kama maelfu ya vijana watazihama nchi zao kwenda kutafuta kaskazini Ulaya na kuwaletea fedha wazee wao nyumbani.Mamilioni ya familia kubwa kubwa wanategemea fedha hizo.Kuwazuwia vijana kutoka linaandika gazeti la Süddeutsche Zeitung " ni sawa na kuzidisha kero na hali ya kuvunjika moyo nchini,hali sawa na ile iliyoshuhudiwa vijana walipoteremka majiani mijini Brazaville,Kinshasa au Bujumbura kulalamika dhidi ya walioko madarakani.Uhamiaji ni sawa na kilango cha kuvutia pumzi kwa serikali ili kupunguza shinikizo la barabarani.Nchi za Ulaya kwa hivyo zisitarajie kwamba wenzao wa Afrika watapania kukabiliana na hali hiyo ambayo upande wa pili tuu wa bahari ya Miditerenia inatajwa kuwa mzozo.Badala yake nchi za Ulaya zinabidi zibadilishe msimamo wake na hasa kuelekea suala la waakimbizi.Vijana wanaofuata jangwa na Sahara na kujitosa katika bahari ya Mediterenia wanazijua vilivyo picha za televisheni zinazoionyesha mashua zilizozama na maiti zinazoelea baharini.Na wanazijua pia hadithi za wale waliofanikiwa barani Ulaya na kupata mishahara mizuri na kuinua maisha ya familia zao nyumbani linamaliza kuandika gazeti la Süddeutsche Zeitung.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/BASIS/PRESSER/ALL

Mhariri: Gakuba Daniel