1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bush na Blair watofautiana juu ya jukumu la Iran na Syria kuelekea Irak

Gregoire Nijimbere14 Novemba 2006

Rais wa Marekani George W. Bush na waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair, wanafikiria sera mpya kuhusu mzozo wa Irak. Lakini wakati waziri mkuu wa Uinegereza Tony Blair akihisi kuwa kuzishirikisha nchi kama Iran na Syria kutaweza kusaidia kuusuluhisha mgogoro huo, rais wa Marekani, George W.Bush ameonekana kutounga mkono wazo hilo.

https://p.dw.com/p/CBI4
Rais wa Marekani, George W. Bush pamoja na waziri mkuu wa Uingereza,Tony Blair
Rais wa Marekani, George W. Bush pamoja na waziri mkuu wa Uingereza,Tony BlairPicha: AP

Rais wa Marekani, George W. Bush ambae anakabiliwa na shinikizo kubwa kutoka kwa wabunge kutoka chama cha demokrate ambao sasa wanalidhibiliti bunge kufuatia ushindi katika uchaguzi wa wiki iliopiota, hakuunga mkono wala kupinga kabisa pendekezo la wabunge hao la kuyaondoa hatua kwa hatua majeshi yake kutoka Irak. Utaratibu huo ungeanza baada ya miezi minne au 6 ijayo kulingana na Karl Levin kutoka chama cha demokrate.

Rais Bush hakuzungumzia sana kuhusu pendekezo hilo lakini akasema tu kuwa haoni kuwa kwa vyovyote vile msaada kutoka kwa Iran au Syria unahitajika katika kuusuluhisha mgogoro wa Irak. Tayari rais Bush anazichukulia nchi hizo za Syria na Iran kuwa ni madui wakubwa wa Marekani na kwamba zinasaidia ugaidi sio tu mashariki ya kati bali pia duniani.

Waziri mkuu wa Uingereza, Tony Blair alisema na hapa ninamnukuu´´ tunaipa Iran chaguo la mkakati wa wazi. Ichangie katika mpango mzima wa kusaka amani ya mashariki ya kati na sio kuukwamisha, isimamishe kuusaidia ugaidi nchini Lebanon au Irak, basi ushirikiano mpya nasi ni jambo linalowezekana´´. Mwisho wa kumnukuu Tony Blair.

Lakini pamoja na kuweko tofauti hiyo ya maoni kati ya viongozi hao wawili Bush na Blair, washirika wawili wakubwa nchini Irak, Tony Blair alikiri kuwa hakuna njia nyingine isipokuwa kushirikiana na Marekani.

Blair amesema:

´´Tunaweza kukubaliana na Marekani au laa kuhusu msimamo wetu juu ya baadhi ya maswala au hata juu ya maswala yote, lakini Uingereza haiwezi kuyasuluhisha maswala yote hayo peke yake, bila Marekani´´.

Rais Bush amekutana jana kwa mazungumzo na kundi linalohusika na taaluma juu ya Irak ambalo litatoa ripoti yake juu ya mzozo wa Irak na maagizo kuhusu usuluhishi wa mzozo huo. Kundi hilo linaongozwa na waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani James Baker na mbunge wa zamani katika jimbo la Indiana kutoka chama cha demokrate, Lee Hamilton.

Baada ya mkutano na rais Bush, Baker alisema na hapa ninamnukuu´´tunayo furaha kwa kuwa tumeweza kuzungumza na viongozi tawala wa Marekani na tunasubiri pia kuzungumza na viongozi wa ngazi ya juu katika chama cha demokrate. Pia tutafanya kila juhudi ripoti yetu itoke mwezi ujao.´´ Mwisho wa kumnukuu James Baker.

Ripoti hiyo inasubiriwa kwa hamu kubwa sana kwa sababu wapigaji kura walionyesha upinzani wao kuhusu sera za rais Bush kuhusu mzozo wa Irak ambao ulichangia kushindwa kwa chama chake cha Republican wakati wa uchaguzi wa bunge tarehe 7 mwezi huu.

Lakini wadadisi wa maswala ya kisiasa wanasema, rais Bush alipinga kuyaondoa majeshi yake kutoka Irak wakati wa kampeni ya uchaguzi huo wa bunge na hawadhani kuwa atabadili masimamo wake.