1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cameron afanya ziara ya ghafla Afghanistan

Mohammed Khelef3 Oktoba 2014

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron aliwasili Afghanistan, akiwa kiongozi wa kwanza wa nje kukutana na Rais Ashraf Ghani, huku vikosi vya NATO vikikaribia mwisho wa vita vyake dhidi ya Taliban.

https://p.dw.com/p/1DPKT
Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron (kushoto), na mwenyeji wake Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan.
Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron (kushoto), na mwenyeji wake Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan.Picha: Reuters/O. Sobhani

Cameron aliwasili kwenye mji mkuu Kabul siku ya Ijumaa (3 Oktoba) katika ziara ambayo haikutangazwa hapo kabla, akitokea kituo cha jeshi la anga la nchi yake kilichoko kwenye kisiwa cha Cyprus, ambako ndege za Uingereza hufanyia mashambulizi yake dhidi ya wanamgambo wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu (IS) nchini Iraq na Syria.

Viongozi hao wawili walikutana na waandishi wa habari baadaye asubuhi, ambapo Cameron alisifu uundwaji wa serikali ya umoja wa kitaifa nchini Afghanistan na kuahidi kuwa Uingereza itaendelea kuiunga mkono Afghanistan katika masuala ya usalama wake, ingawa jitihada zaidi zinapaswa kufanywa na Waafghani wenyewe.

"Kwa usahihi zaidi ni kuwa kombora linaweza kumuua gaidi, lakini ni utawala bora ndio unaoua ugaidi. Kwa hivyo jambo linalohitajika sana ni kwa serikali hii mpya ya umoja wa kitaifa kuiunganisha nchi," alisema Cameron.

Cameron alisema Uingereza ilijitolea pakubwa kwenye kusaidia kuleta utulivu wa Afghanistan, akikumbushia wanajeshi 453 wa nchi yake ambao wamekufa wakihudumu nchini Afghanistan. Alitazamiwa pia kuwatembelea wanajeshi 3,900 wa kwenye jimbo la Kandahar, ambao wameendelea kusalia Afghanistan ikiwa sehemu ya kikosi kinachoongozwa na Jumuiya ya Kujihami ya NATO.

Muda wa mwisho wa NATO wakaribia

Kwa ujumla, jeshi la Uingereza limekamilisha uwepo wake kwenye jimbo tete la Helmand kusini mwa Afghanistan baada ya miaka kadhaa ya mapigano na katika wiki za hivi karibuni, wanamgambo wa Taliban wameanzisha hujuma mpya kwenye maeneo hayo.

Ndege za kijeshi za Uingereza kwenye kituo chake nchini Cyprus.
Ndege za kijeshi za Uingereza kwenye kituo chake nchini Cyprus.Picha: Reuters/Cpl Neil Bryden/Ministry of Defence

Rais Ghani Ahmadzai aliapishwa siku ya Jumatatu, akianza uongozi mpya wa nchi hiyo chini ya serikali ya umoja wa kitaifa, yenye jukumu kubwa la kuwakabili wapiganaji wa Taiban, ambao licha ya vita vya miaka 13 kutoka madola makubwa duniani, wameendelea kuwa na nguvu.

Siku moja baada ya kuapishwa kwake, serikali yake ilisaini mkataba wa usalama unaoiruhusu Marekani kuendelea kubakisha wanajeshi takribani 10,000 ili kusaidiana na vikosi vya usalama vya Afghanistan.

Makubaliano mengine kando ya hayo yalisainiwa kuruhusu kati ya wanajeshi wengine 4,000 hadi 5,000 wa NATO, wengi wao kutoka Uingereza, Ujerumani, Italia na Uturuki kuendelea kubakia hata baada ya operesheni ya NATO kumalizika tarehe 31 Disemba mwaka huu.

Mtangulizi wa Rais Ghani, Hamid Karzai, alikuwa amekataa kusaini makubaliano hayo, akitaka sharti la kuwawekea kinga ya kutoshitakiwa wanajeshi wa kigeni iondolewe.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/AP
Mhariri: Josephat Charo