1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cameroon kucheza katika Kombe la Dunia

18 Novemba 2013

Cameroon imejikatia tikiti za ndege kuelekea Brazil mwakani, baada ya kusajili ushindi mkubwa wa magoli manne kwa moja dhidi ya Tunisia mjini Yaounde katika mkondo wa pili wa mechi ya mchujo hapo jana.

https://p.dw.com/p/1AKFV
Picha: Fethi Belaid/AFP/Getty Images

Timu hizo mbili zilitoka sare ya bila kufungana katika mkondo wa kwanza nchini Tunisia. Sasa The Indomitable Lions wanaungana na Nigeria na Cote d'Ivoire ambazo zilishinda mechi zao za mchujo hapo Jumamosi, na kufungasha virago kuelekea Brazil. Cote d'Ivoire walitoka sare ya kufungana goli moja kwa moja dhidi ya Senegal ambalo na hivyo ikafuzu kwa jumla ya magoli manne kwa mawili mjini Casablanca, Morocco.

Mapema, The Super Eagles, walifuzu kwa mara ya tano katika tamasha hilo baada ya kuwapiku Ethiopia mabao mawili kwa sifuri nyumbani Calabar, na hivyo kupata jumlaya magoli manne kwamoja.

Timu mbili za Afrika zilizobaki zitajulikana hapo kesho Jumanne, wakati Misri ikihitaji muujiza mkubwa katika kujaribu kubatilisha kichapo cha mkondo wa kwanza cha magoli sita kwa moja dhidi ya Ghana.

Lakini vita vikali vitakuwa katika mchuano kati ya wenyeji Algeria na Burkina Faso katika uga wa Mustapha Tchaker mjini Blida, ambako Algeria haijawahi kupoteza katika michuano 19 tangu mwaka wa 2002. Burkina Faso wana faida ya magoli matatu kwa mawili kutokana na mkondo wa kwanza.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters

Mhariri:Yusuf Saumu