1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CAN 2010 ANGOLA:Vigogo zaidi vyaangushwa

14 Januari 2010

Maajabu katika michuano hiyo ya mataifa ya Afrika kwa vigogo kuangushwa au kubanwa yaliendelea kujitokeza , pale Simba wanyika Cameroon walipolambishwa mchanga na Gabon huku Tunisia wakibanwa na Zambia.

https://p.dw.com/p/LVLL
Kombe la mataifa ya Afrika 2010 Angola

Katika mechi  hizo za Kundi D ziilizofanyika kwenye  mji wa Lubango, Cameroon moja ya timu vigogo barani Afrika na ambayo ikipigiwa upatu, kutoroka na kombe, ilipata kipigo kutoka kwa Gabon baada ya kuchapwa bao 1.0.

Kipigo hicho kwa Cameroon kinaifanya kuwa timu ya tatu kati ya tano zitakazoiwakilisha Afrika katika fainali za dunia mwezi wa sita nchini Afrika Kusini, kufungwa katika michuano hiyo ya Angola.

Nyingine ni Nigeria iliyoshindiliwa mabao 3-1 na mabingwa watetezi Misri, pamoja na Algeria ambayo ilikiona cha mtema kuni mbele ya Malawi kwa kukandikwa mabao 3-0.

Simba Wanyika Cameroon ambao katika mbio za kuwania tiketi ya kwenda Afrika Kusini, walikuwa kundi moja na Gabon na kuwafunga mechi zote mbili, sasa wanawajibika kuwafunga Zambia hapo siku ya Jumapili, kabla ya kukutana na Tunisia, ili kufufua matumaini ya kusonga mbele.

Simba mkongwe Rigobert Song aliweka rekodi kuwa mchezaji wa kwanza kucheza fainali nane za mataifa ya Afrika, lakini hata hivyo alidhihirisha kuwa misuli yake imechoka pale aliposhindwa kumbana Roguy Meye, aliyetoa pasi kwa Daniel Cousin anayechezea Hull City ya Uingereza kuweza kuipatia Gabon bao hilo muhimu.

Kocha wa Cameroon mfaransa Paul Le Guen, alikiri kuwa walicheza chini ya kiwango chao.Lakini nahodha wa timu hiyo, Samuel Eto´o alisema kuwa mara zote huwa wanaanza vibaya na kumaliza vizuri, akikumbushia fainali zilizopita nchini Ghana, ambapo walipoteza mechi ya kwanza, lakini katika mechi ya pili dhidi ya Zambia walishinda na kusonga mbele.Ni Zambia hiyo hiyo wanayokumbana nayo tena Jumapili.

Kwa upande wake kocha wa Gabon, nyota wa zamani wa Ufaransa Alain Giresse alisema kuwa wamefurahishwa sana na matokeo hayo, na kwamba mfumo wao wa kucheza kiufundi ulikuwa mzuri sana.Amesema kuwa ndoto yao sasa ni kufuzu kwa robofainali, hata kama watashika nafasi ya pili, haijalishi.

Kwa upande mwengine Tunisia ambao mwaka 2004 walitwaa ubingwa huo wa mataifa ya Afrika,sasa wanawalazimika kuifunga Gabon katika mechi ijayo ili kujiweka katika nafasi ya kufuzu kwa robofainali, baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Zambia.

Zambia ilikuwa ya kwanza kupachika bao katika dakika ya 19, kupitia kwa mchezaji wao anayesukuma kandanda la kulipwa nchini Uholanzi, Jacob Mulenga, kufuatia pasi ya James Chamanga anayecheza soka la kulipwa nchini China.

Tunisia walisawazisha bao hilo dakika tano kabla ya mchezo baada ya Youssef Msakni kuichambuangone ya Zambia kutoka wingi ya kushoto na kumuachia uwanja Zouhaier Dhaouadhi kusawazisha bao hilo.

Kocha wa Zambia, Herve Renard, alilaumu kwa kushindwa kuondoka na pointi zote tatu, akisema kuwa baada ya kupata bao la kuongoza wachezaji wake walishindwa kuonesha nidhamu zaidi dimbani na kutoa mwanya kwa Tunisia kusawazisha.

Mwenzake wa Tunisia Faouzi Benzarti aliwapongeza vijana wake akisema kuwa wangeweza kutoka na ushindi hususan kutokana na jinsi walivyotandaza soka katika kipindi cha pili, lakini akasema sare hiyo inastahiki.

Leo mjini Luanda, wenyeji Angola katika kundi A wanakumbana na Malawi, ambayo inachagizwa na ushindi wake wa kwanza dhidi ya Algeria, huku Mali ikikumbana na Algeria.

Katika mechi ya kwanza ya kundi hilo, Angola ilishindwa kulinda vyema mlango wake na kushuhudia Mali ikisawazisha mabao manne, na kuufanya mpambano umalizike kwa sare ya mabao 4-4.

Malawi ndiyo inayoongoza kundi hilo ikiwa na pointi tatu na hivyo kuhitaji ushindi mwengine au pengine sare kujiweka katika nafasi ya kufuzu kwa robofainali.

Pembezoni mwa dimba huko huko Angola, kocha wa Nigeria Shaibu Amodu, yuko katika mbinyo mkubwa wa kutaka atimuliwe , kufuatia kipigo ambacho timu hiyo imekipata katika mechi ya kwanza dhidi ya Misri.

Hata hivyo kocha huyo mwenye umri wa miaka 51 amesema kuwa hasumbuliwi na shutuma hizo kutoka kwa washabiki nchini Nigeria za kumataka atimuliwe na kwamba anatilia maanani mechi yake ya pili dhidi ya Benin hapo siku ya Jumapili.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/Reuters