1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CAN 2010:Algeria na kina Drogba waduwazwa

12 Januari 2010

Leo mazungmzo katika anga ya spoti ni matokeo ya mechi za jana.Malawi kuibanjua Algeria, na Bukina Faso kuisimamisha Ivory Coast

https://p.dw.com/p/LRN1
Kombe la mataifa ya Afrika 2010 nchini AngolaPicha: AP

Ushindi wa Malawi wa mabao 3-0 dhidi ya Algeria hapo jana umewaduwaza wengi.Algeria ambayo ni moja kati ya timu tano zitakazoiwakilisha Afrika katika fainali zijazo za kombe la dunia, ilijikuta katika wakati mgumu mbele ya Malawi.

Kipigo hicho kilichotolewa na Malawi ambayo mara ya mwisho kushiriki katika fainali hizo za Afrika ilikuwa mwaka 1984, kimewapa shaka kubwa washabiki wa kabumbu barani Afrika juu ya uwezo wa Algeria kuliwakilisha bara la Afrika nchini Afrika Kusini katika kombe la dunia.

Kiungo wa timu hiyo ya Malawi Joseph Kamwendo mara baada ya mechi hiyo mjini Luanda alisema kuwa wao ndiyo timu pekee ambayo haipewi matumaini yoyote ya kufika mbali, lakini wao wenyewe wana mikakati ya kulifuta hilo, na wamedhihirisha.

Kwa upande wake kocha wa Algeria Rabah Saadane alilalamikia hali ya joto kali, kuwa ilichangia kufungwa kwao na kuwataka waandaji kupanga mechi nyingine katika muda ambao joto litakuwa limepungua.

Hata hivyo kiungo wa timu hiyo Rafiki Saifi alijipa moyo akisema kuwa ni bora kufungwa mechi moja mabao 3-0 kuliko kufungwa mechi tatu bao1-0 kila mmoja, na kwahivyo bado wana nafasi ya kusonga mbele kwani kuna mechi mbili mbele yao.

Katika mji wa Cabinda uliyoshuhudia shambulio dhidi ya timu ya Togo lililofanywa na waasi wanaotaka kujitenga kwa jimbo hilo, Tembo wa Ivory Coast wanaopigiwa upatu mkubwa kutwaa kombe hilo, walijikuta wakilazimishwa kutoka suluhu bin suluhu na Bukina Faso katika mechi ya kwanza ya kundi B.

Mechi ya kwanza katika kundi hilo ilikuwa iwe kati ya Togo na Ghana, lakini kutokana na kujitoa kwa Togo sasa kundi hilo limebakia na timu tatu tu.

Shirikisho la soka Barani Afrika CAF limetangaza kuiondoa kabisa Togo katika fainali hizo, baada ya kuondoka hapo juzi kurejea nyumbani kutokana na tukio la kushambuliwa na waasi.

Tembo wa Ivory Coast wakiwa na majogoo kadhaa  wanaowika katika dimba duniani, kama vile Didier Drogba na ndugu wawili Kolo na Yaya Toure walishindwa kupata ufunguo wa kufungua lango la Bukina Faso pamoja na kwamba walipiga hodi mara kadhaa mlangoni hapo.

Drogba alisema kuwa ilikuwa vigumu kulifungua  lango la timu hiyo ambayo ilipania kulilinda lango lao kwa kila hali, na kwamba matokeo hayo yanawaweka pagumu.

Yaya Toure alikubaliana na Drogba kuwa pointi moja waliyoipata hiyo jana inawaweka katika wakati mgumu na kwamba wamechanganyikiwa na matokeo hayo, kwani sasa wanawajibika kuifunga Ghana katika mechi ijayo hapo siku ya Ijumaa.

Leo hii mabingwa watetezi Mafarao wa Misri wakiwa na hasira ya kuikosa tiketi ya kucheza katika fainali za dunia, wataanza safari ya kuutetea uchampion wao kwa kuvaana na Nigeria, katika mechi ambayo inatarajiwa kuwa ngumu, kali na ya kuvutia.Mechi hiyo itafuatiwa na mechi ya kundi C katika mji wa Benguela kati ya Msumbiji na Benin.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/Reuters

Mhariri:Othman Miradji