1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cancun: Marekani na China vidole machoni

Admin.WagnerD30 Novemba 2010

Huku Marekani na China zikidai kupigwa kwa hatua katika mzozo wao wa uzalishaji wa hewa chafu, bado pana hali ya kutokaminiana baina yao na pia kutokuaminiwa wote wawili na ulimwengu.

https://p.dw.com/p/QLpo
Walinda Mazingira wakirusha puto lenye maandishi "Okoa Mazingira" na "Zuia Kupanda kwa Joto la Dunia" juu ya mabaki ya mji wa kale wa Mayan city of Chichen Itza, tarehe 28 Novemba 2010
Walinda Mazingira wakirusha puto lenye maandishi "Okoa Mazingira" na "Zuia Kupanda kwa Joto la Dunia" juu ya mabaki ya mji wa kale wa Mayan city of Chichen Itza, tarehe 28 Novemba 2010Picha: picture alliance/dpa

Marekani na China ambazo ndizo nchi zenye uchumi mkubwa duniani na nchi zinazotoa gesi nyingi inayochafua mazingira, zimelaumiana kwa kutowajibika vilivyo kupambana na hali ya Ujoto duniani mwaka huu, na hili limechangia kusita kwa mazungumzo ya Umoja wa mataifa miongoni mwa takriban mataifa 200.

Mkuu wa ujumbe wa Marekani katika mkutano huo wa Cancun,Jonathan Pershing, amesema kwamba nguvu nyingi zimetumika katika mwezi uliopita kuyashughulikia masuala hayo ambayo wanatofautiana na China na wanajaribu kuyatatua.

Mazungumzo hayo yanayofanyika katika hoteli iliyo chini ya ulinzi mkali mjini Cancun, yanatafuta njia za kufufua majadiliano baada ya mkutano wa Umoja wa mataifa uliofanyika Copenhagen, na ulioshindwa kufikia makubaliano kwa kuidhinisha mkataba wa pamoja, mwaka uliopita.

Umoja wa mataifa unataka makubaliano kuhusu hazina ya kimazingira itakayozisaidia nchi zinazoendelea pamoja na njia za kuhifadhi misitu na kuwasaidia maskini kuzoea hali ya ujoto inayozidi. Mkutano huu pia unalenga kuyafanya rasmi malengo ya kuzuia utoaji wa gesi zinazochafua mazingira.

Mkuu wa Ujumbe wa China Su Wei alikuwa muangalifu zaidi kuhusu suala la kupatikana maendeleo katika mzozo huo.

Alisema kwamba mazungumzo kati ya nchi yake na Marekani yalikuwa ya wazi na kwamba pande zote zingependa kuona matokeo mazuri mwishoni mwa mkutano huo wa Cancun.

Tabia nchi ni mojawapo ya mizozo kati ya nchi hizo mbili zenye uchumi mkuu, pamoja na masuala ya biashara na viwango vya ubadilishaji wa sarafu.

Mkutano wa matayarisho wa Umoja wa Mataifa kuhusu tabia nchi uliofanyika nchini China mnamo mwezi Oktoba mwaka huu, uligubikwa na mizozo kati ya nchi hiyo na Marekani.

Pershing amesema kwamba rais wa Marekani Barack Obama, ameahidi kupunguza viwango vya gesi hizo nchini Marekani, vilivyokuwepo mwaka 2005, kwa asilimia 17 kufikia mwaka 2020, licha ya chama cha Republican nchini humo kushinda kwa wingi wa kura katika uchaguzi uliofanyika mwezi Novemba.

Mkutano huo wa Cancun awali ulifunguliwa kwa kutolewa wito wa kuchukua hatua za kuzuia athari zaidi zinazotokana na mafuriko, ukame, kiangazi,na kupanda kwa viwango vya bahari.

Mkutano huu utawajumuisha zaidi ya mawaziri 100 wa mazingira na kiasi cha mawaziri wakuu na marais 25 wiki ijayo.

Mwandishi: Maryam Abdalla/RTRE

Mhariri: Mtullya Abdu