1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CARACAS : Chavez ashinda uchaguzi wa rais

4 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CCmq

Mpinzani mkubwa wa Marekani Rais Hugo Chavez wa Venezuela anaelekea kushinda uchaguzi wa rais uliofanyika nchini humo hapo jana.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni wa matokeo ya awali ya uchaguzi huo Chavez amejizolea asilimia 61 ya kura dhidi ya mpinzani wake gavana wa jimbo Manuel Rosales aliyejipatia asilimia 38.

Mamia ya wafuasi wa rais huyo wa sera za mrengo wa shoto walimiminika mitaani kusheherekea kwa kuwasha fataki na kucheza kwa mdundo wa nyimbo za kumuunga mkono Chavez zilizokuwa zikihanikizwa kutoka vipaza sauti vya magari makubwa ya mizigo.

Chavez mwenye umri wa miaka 52 anayejiita mtetezi wa maskini ambaye ameiongoza Venezuela kwa miaka minane ameapa kuendeleza sera zake za kimapinduzi na kusema kwamba atauleta ujamaa wa karne ya 21 kwa nchi yake hiyo ya Amerika ya Kusini yenye utajiri wa mafuta.

Mpizani wake Manuel Rosales aliahidi kumshinda Chavez ambaye anamshutumu kwa kuielekeza Venezuela kwa mtindo wa utawala wa mtu mmoja wa Cuba.