1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama tawala cha Tanzania chapata nguvu mpya kwa Magufuli

Anaclet Rwegayura1 Septemba 2015

Gumzo katika kila mji na kijiji nchini Tanzania ni juu ya uchaguzi mkuu ujao na uchaguzi wa rais. Katika barua yake ya mwezi Julai, mwandishi wa DW Anaclet Rwegayura anasema Magufuli anaipa CCM tija.

https://p.dw.com/p/1GPdp
John Magufuli
Picha: picture-alliance/AP Photo/K. Said

Matokeo ya chaguzi ambayo ni uundaji wa serikali, bunge na serikali za mitaa huwa jambo lenye mvuto kwa kila raia. Na zaidi huwatia shauku wale wanaotafuta manufaa ya madaraka pamoja na wale wanaojikomba kwa wale ambao wanadhaniwa watakuwa washindi katika uchaguzi. Baada ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kutangaza tarehe 12 Julai mgombea wake wa urais, siyo kwamba kazi imekamilika. Hata hivyo homa ya kisiasa iliyokuwa imegubika taifa imeanza kushuka.

Ikiwa matokeo ya kura ya 25 Oktoba 2015 hayakuleta habari tofauti na ya kushangaza, Waziri wa Kazi John Pombe Magufuli anayesifiwa kwa kutovumilia upuuzi, ni mtu anayekubalika kwa Watanzania wapiga kura ambao sasa wamechoshwa zaidi na rushwa kuliko maradhi yoyote, mbali ya uzembe na uwajibikaji hafifu katika asasi za umma.

Wapiga kura wameelimika

Taifa hili linahitaji mtu atakayeweza kuweka mazingira ya uongozi ambayo hayaruhusu watu wanaojikomba kwa viongozi au kuleta michezo ya kisiasa ili kufunika uzembe, bali kuhimiza ufanisi na uwajibikaji katika kazi za serikali na utawala wa dola.

Yako mambo mengi yanayoikabili Tanzania wakati huu. Kwa sababu hii, wapiga kura, ambao wamejitokeza kwa wingi kujiandikisha kwa ajili hiyo, wanataka wawe na hakika kwamba wale wanaowania uchaguzi kutoka vyama vyote vya siasa watatengeneza sera za kuondoa kero zilizopo sasa, na mwisho wa siku, waonyeshe matokeo.

Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania amaliza muda wake wa uongozi
Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania amaliza muda wake wa uongozi wa miaka 10Picha: DW / Khelef Mohammed

Hapana shaka kwamba raia wanaelewa haki zao za uchaguzi. Tanzania hairuhusu wahamiaji na wananchi wake waishio ughaibuni kupiga kura. Wapiga kura wanataka kusikia katika midahalo ya kampeni za wawania uchaguzi, ambao wameteuliwa na vyama vyao vya siasa, matamko ya busara na siyo kelele za jeuri kuhusu vipaumbele vya majimbo na taifa kwa jumla.

Katika harakati za kutafuta uteuzi kwa vyama vyao, baadhi ya watu tayari wanazunguka huku na kule katika majimbo, wanajitokeza karibu popote palipo na mkusanyiko wa watu na hata kutembelea wagonjwa wasiowafahanu ambao wamelazwa hospitalini ili wapate kuungwa mkono na sehemu kubwa ya jamii.

Magufuli apunguza kasi ya wagombea wengine

Wale wanaowania uchaguzi kwa mara ya kwanza huenda wakawa wengi baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuongeza majimbo mapya, baadhi ya vyama kujitokeza vile vile tangu uchaguzi mkuu uliopita na idadi ya watakaopiga kura kwa mara ya kwanza kuongezeka.

Kupitia mgombea wake wa urais Magufuli, CCM kimepunguza kasi ya vyama vya upinzani kwa sababu huyu ni mtu ambaye Watanzania wengi wanakiri kwamba atamzidi kila mshindani ambaye huenda akateuliwa na vyama vya upinzani.

Lakini katika Tanzania yenye demokrasia uwanja bado ni wazi kabisa kwa chama choichote kujitahidi ili kiibuke na ushindi mkubwa katikia Bunge na halmashauri za wilaya na manispaa.

Chama tawala kimetoa ilani yake ya uchaguzi. Vyama vingine vinavyotaka kuingia katika kinyang’anyiro hicho hapana budi vitangaze pia ilani zao na kuweka tayari mikakati yao ya kampeni, bila kusahahu kundi kubwa la vijana watakaopiga kura kwa mara ya kwanza.

Takwimu za idadi ya watu nchini zinaonyesha kuwa kundi hili linaweza kuwa na msukumo mkubwa katika uchaguzi kuanzia kura za maoni ambazo huamua nani watakaosimama katika uchaguzi mkuu.

Inasikitisha kuona watu wakiyumba

Hali ya watu kutojali kwa kiasi fulani iliathiri matarajio ya umma katika chaguzi zilozopita. Sababu mbalimbali zilichangia hali hiyo na baadhi ya hizo ni uteuzi wa wagombea wasiopendelewa na wapiga kura, rushwa na uongozi wa zoezi la uchaguzi ambao ulisukumwa na matakwa ya baadhi ya watu.

Pamoja na mambo hayo, ufuatiliaji wa vyombo vya habari au kutofuatilia wagombea uchaguzi wa urais na ubunge daima huwa na msukumo kwa wapigakura Watanzania. Ni jambo la kusikitisha kuona wakati uchaguzi unapokaribia baadhi ya sehemu za jamii au watu binafsi wanayumba kutokana na hadithi zinazotangazwa na vyombo vya habari na kufanya uchaguzi wa ovyo, bila kufanya jitihada ya kupata ukweli.

Kwa jumla Watanzania wanaelewa taarifa za habari za upendeleo na matokeo yake katika chaguzi za nchi jirani. Kwa hiyo vyombo vya habari nchini hapana budi vitoe maoni huru na vijiepushe na taariri ambazo huenda zikapotosha umma.