1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha Bhutto chatafakari kujiondoa katika uchaguzi

30 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/Chz3

Chama cha Pakistan Peoples Party, PPP, kinakutana hii leo kufuatia kuuwawa kwa kiongozi wake, waziri mkuu wa zamani Benazir Bhutto, ili kuamua ikiwa kitashiriki katika uchaguzi uliopangwa kufanyika nchini Pakistan tarehe 8 mwezi ujao wa Januari.

Chama cha PPP pia kitasikiliza wosia wa marehemu Bhutto, huku kukiwa na hali ya kutatanisha kuhusu kifo chake.

Serikali ya Pakistan imekataa msaada wa kigeni katika kuchunguza kifo cha Benazir Bhutto.

Kundi la wanamgambo wa kiislamu lililotajwa kuhusika na mauaji ya kiongozi huyo limepinga kuhusika na njama ya kumuua, na wapambe wa Benazir Bhutto wameilaumu serikali kwa kujaribu kufunika ukweli.

Kujiondoa kwa chama cha Pakistan Peoples Party kushiriki katika uchaguzi wa Januari 8 kutavuruga uhalali wa uchaguzi huo, ambao tayari umegomewa na chama cha kiongozi mwengine wa upinzani nchini Pakistan, Nawaz Sharif.