1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha Ennahda chaongoza katika uchaguzi Tunisia

24 Oktoba 2011

Shughuli ya kuhesabu kura inaendelea nchini Tunisia kufuatia uchaguzi wa kihistoria kufanyika tangu kuanza kwa wimbi la mapinduzi ya raia katika nchi za kiarabu.

https://p.dw.com/p/12xnI
Raia wa Tunisia wapeperusha bendera ya nchini humoPicha: picture-alliance/dpa

Kulingana na vyombo vya habari nchini humo, ambavyo vilikuwa vinatangaza baadhi ya matokeo ya uchaguzi huo huru uliofanyika hapo jana, chama cha kiislamu cha Ennahda kinaongoza kwa wingi wa kura.

Hata hivyo tume ya uchaguzi nchini Tunisia inatarajiwa kutoa matokeo rasmi ya uchaguzi baadaye hapo kesho.

Mwanachama wa baraza la Ennahda, Ali Marayedh amesema anaamini tayari chama hicho kimechukua ushindi.

Marayedh amesema chama cha Ennahda kinaongoza kwa kura kati

ya asilimia 25 na 50 kulingana na jimbo la uchaguzi.

Barack Obama im Weißen Haus zum Ende des Irakkrieges
Rais Barack Obama wa MarekaniPicha: dapd

Tayari mataifa ya magharibi yameupongeza uchaguzi huo yakiwemo Marekani na Umoja wa Ulaya walioipongeza tuniasia kwa uchaguzi wa amani.

Rais Barack Obama amesema uchaguzi huo ni hatua muhimu sana kwa kupatikana amani na demokrasia nchini Tunisia.

Raia nchini humo nao walikuwa na raha wakisema hii ni hatua

muhimu kufungua ukurasa mpya wa demokrasia nchini  Tunisia.

Vyama 77 vilishiriki katika uchaguzi huo wa kwanza ulio huru nchini Tunisia. Uchaguzi huo uliofanyika kuwachagua wajumbe 217, watakayojishughulisha na mchakato mzima wa kuandika katiba mpya na vile vile kuteua serikali mpya ya mpito.

Raia wengi nchini Tunisia walijitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi huu wa kwanza huru na wa kihistoria uliofanyika miezi tisa tangu kufanyika wimbi la mapinduzi ya raia yaliyomshinikiza rais wa zamani Ben Ali aliyetawala nchi hiyo kwa miaka 23, kuondoka madarakani, na kukimbilia mafichoni nchini Saudi Arabia.

Tunisia ndio iliyoanzisha wimbi la mapinduzi ya raia katika nchi za kiarabu.  Raia nchini humo waliandamana kupinga umaskini, ukosefu wa ajira na ukandamizaji wa serikali.

Mkuu wa tume ya uchaguzi nchini Tunisia, Kamal Jendoubi, jana alisema zaidi ya asilimia 90 ya watu milioni 4.1 waliosajiliwa walipiga

kura.

Mwandishi Amina Abubakar/RTRE/ DPA Mhariri Josephat Charo