1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha PP chakosa viti vya kutosha kuunda serikali

27 Juni 2016

Kaimu Waziri Mkuu wa Hispania Mariano Rajoy amesema ataweka msukumo wa kushika madaraka ya uongozi wa taifa hilo baada ya chama chake cha kihafidhina cha Popular Party kushinda viti zaidi katika uchaguzi wa bunge.

https://p.dw.com/p/1JEI2
Kiongozi wa chama cha Peoples Party nchini Hispania, Mariano Rajoy
Kiongozi wa chama cha Peoples Party nchini Hispania , Mariano RajoyPicha: Reuters/J. Medina

Uchaguzi huo ambao umefanyika kwa mara ya pili katika kipindi cha miezi sita unakuja mnamo wakati Umoja wa Ulaya ukiwa katika kipindi cha mpito baada ya Uingereza kupiga kura ya kuamua kujiondoa katika Umoja wa huo.

Chama hicho cha kihafidhina cha PP ambacho kilijinasibu kuwa mlinzi wa uthabiti wa nchi hiyo kilishinda viti 137 katika bunge la nchi hiyo lenye jumla ya viti 350 vikiwa ni viti 14 zaidi kulinganisha na viti ambavyo kilipata katika uchaguzi wa mwezi Disemba mwaka jana na pia kuliko ilivyotarajiwa.

Chama cha Sosholisiti kilishika nafasi ya pili kikipata viti 85 yakiwa ni matokeo mabaya zaidi kwa upande wake katika miaka ya hivi karibuni.

Chama cha mrengo wa kushoto cha Unidos Podemos kilishika nafasi ya tatu katika uchaguzi huo kikipata viti 71 kinyume cha matarajio ya awali kuwa chama hicho kingefanya vizuri zaidi na kukishinda chama cha mrengo wa kushoto cha wasosholisti.

Chama kinachopendelea masoko cha Ciudadanos kilishika nafasi ya nne kikipata viti 32, ikiwa ni pungufu kutoka viti 40 kilichopata awali kufuatia wapiga kura wengi kurejea katika chama cha PP.

Chama cha PP chadai mamlaka kamili

Tumeshinda na hivyo tunahitaji haki yetu ya kuongoza serikali , ilikuwa ni vigumu kupata ushindi lakini hata hivyo tunapigania taifa " alisikika Rajoy wakati mkononi akiwa ameshika bendera yenye rangi ya bluu.

Baadhi ya wabunge wakiwa ndani ya bunge nchini Hispania.
Baadhi ya wabunge wakiwa ndani ya bunge nchini Hispania.Picha: Lauren Frayer

Licha ya chama cha PP kuongeza idadi ya viti katika uchaguzi huo bado kinakabiliwa na changamoto kutokana na kutokuwa na idadi ya kutosha ya viti vinavyokipa nguvu ya kuunda serikali.

Hata kama idadi ya viti ambavyo chama cha Ciudadanos kimepata katika uchaguzi huo wa jumapili ikijumulishwa pamoja na idadi ya viti vya chama hicho cha kihafidhina bado itakuwa haitoshi kuwezesha kuunda serikali hivyo chama hicho kitalazimika kukishirikisha chama cha Socialist au vyama vingine.

Chama cha Peoples Party chakabiliwa na kashifa ya rushwa

Hata hivyo vyama vingine vimekuwa vikisita kukiunga mkono chama hicho cha kihafidhina cha PP katika kuunda serikali kutokana na maelezo kuwa chama cha PP kinakabiliwa na kashifa nyingi za rushwa na pia kusababisha ongezeko la watu wasio na ajira ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua kali za kubana matumizi ya umma.

Mmoja wa viongozi wa chama cha Sosholisti nchini Hispania, Pedro Sanchez
Mmoja wa viongozi wa chama cha Sosholisti nchini Hispania, Pedro SanchezPicha: Reuters/J. Medina

Baada ya kushindwa kuunda serikali katika chaguzi tatu ambazo zimekwisha fanyika viongozi wa kisiasa nchini humo safari hii wanakabiliwa na mbinyo unao walazimu kuhakikisha kuwa nchi hiyo inaongozwa na serikali iliyochaguliwa.

Gazeti moja la kila siku nchini humo la El Pais ambalo lina uzwa kwa wingi zaidi kuliko magazeti mengine nchini humo na ambalo liko karibu zaidi na chama cha Socialist katika tahariri yake hii leo limetoa mwito kwa chama cha Socialist kutoa mwanya kwa chama cha PP kuunda serikali.

"Ili serikali iweze kuundwa chama cha Socialist kinapaswa kuheshimu uamuzi wa wapiga kura wengi na hivyo kutoa nafasi ya chama ambacho kina nafasi zaidi ya kuongoza kufanya hivyo kuunda na chenyewe kuendelea kubaki kama chama cha upinzani" Limeandika gazeti hilo.

Uchaguzi huo wa mara ya pili ilikuwa ni lazima ufanyike kutokana na vyama vya kisiasa nchini humo kushindwa kuunda serikali ya mseto baada ya uchaguzi uliofanyika mwezi Disemba mwaka jana na tangu wakati hao Hispania imekuwa haina uongozi wa serikali iliyochaguliwa.

Mwandishi : Isaac Gamba/AFPE/DPAE

Mhariri :Yusuf Saumu