1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha madereva wa treni chaahirisha migomo

6 Januari 2008
https://p.dw.com/p/Ckvx

Chama cha madereva wa treni hapa Ujerumani, GDL, kimekubali kuahirisha migomo iliyopangwa kuanza hapo kesho. Chama hicho pia kimekubali kuendelea mbele na mazungumzo kuhusu mishahara na shirika la usafiri wa reli, Deutsche Bahn, keshokutwa Jumanne.

Chama cha GDL, ambacho kimefanya migomo ya usafiri wa treni za abiria na mizogo tangu mwezi Julai mwaka uliopita, kilikuwa kimetishia kufanya migomo mpaka pande hizo mbili zifikie makubaliano katika mazungumzo yaliyoanza mwezi Machi mwaka jana.

Kiongozi wa chama cha GDL, Manfred Schell, amesema pande hizo mbili zinakaribia kufikia makubaliano kuhusu maswala muhimu kwenye mazungumzo yaliyoandaliwa na waziri wa uchukuzi wa Ujerumani, Wolfgang Tiefensee.

Kiongozi huyo hata hivyo amekiri kwamba hawajafikia lengo lao huku kukiwa na hali ya kutoelewana kuhusu kiwango cha mishahara ya madereva wa treni na saa za kufanya kazi. Hata hivyo bwana Schell amesema ana matumaini wanaweza kufikia makubaliano ifikapo tarehe 31 mwezi huu wa Januari.