1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha Merkel chafikia makubaliano katika majimbo mawili

Sekione Kitojo
14 Juni 2017

Chama  cha  kihafidhina cha  kansela  Angela Merkel CDU kimefikia makubaliano kuunda  serikali  za  mseto  katika  majimbo  mawili muhimu  nchini  Ujerumani.

https://p.dw.com/p/2ehwl
Reaktion auf Prognose Landtagswahl NRW Freude bei CDU
Wafuasi wa chama cha CDU wakishangiria baada ya ushindi katika jimbo la North Rhine WestphaliaPicha: Reuters/T. Schmuelgen

Uchaguzi katika  majimbo  hayo  unaweza kuwa  dalili  ya  kile  kinachoweza  kutokea  katika  uchaguzi  mkuu mwezi  Septemba , ambapo Merkel  anawania  muhula wa  nne madarakani.

Wiki  nne  baada  ya  kupata  ushindi na  wingi usiotarajiwa  katika jimbo  la  North Rhine Westphalia, chama  cha  kansela  wa Ujerumani  Angela  Merkel  cha  Christian Democratic Union CDU pamoja  na  chama  kinachoelemea  upande  wa  wafanyabiashara cha  Free Democrats  FDP vimefikia  makubaliano  kuunda  serikali katika  jimbo  hilo  lenye  wakaazi  wengi  zaidi  nchini  Ujerumani.

Düsseldorf NRW CDU-Chef Armin Laschet Reaktion nach Landtagswahl
Armin laschet mwenyekiti wa CDU jimbo la North Rhine WestphaliaPicha: Reuters/K. Pfaffenbach

"Makubaliano  ya  kuunga  muungano yamekamilika" amesema mwenyekiti  wa  jimbo  wa  chama  cha  CDU Armin Laschet baada ya  duru  ya  saba  ya  majadiliano  katika  muda  wa  wiki tatu. Makubaliano  hayo  yanatarajiwa  kuwekwa  wazi  siku  ya  Ijumaa.

Kubwa  miongoni mwa  makubaliano  kadhaa  ni mtazamo  wa "kutovulimia  kabisa" katika  suala  la  usalama. Mipango  hiyo inajumuisha  upanuzi wa  uchunguzi  kupitia  kamera za  vidio  pamoja na  jeshi  la  polisi.

Infografik Sitzverteilung NRW Landtag 2017 DEU
taswira ya kiwango ambacho kila chama kimepata katika uchaguzi wa North Rhine Westphalia

"Bado tuna  kazi  ya  kufanya , lakini  masuala  makuu  muhimu yamekwisha tatuliwa," amesema  kiongozi  wa  chama  cha  FDP Christian Lindner. baina  yao , vyama  hivyo  viwili  vina  viti 100 kati  ya  viti 199  katika  bunge  la  jimbo  hilo , Landtag.

Laschet atawania  kuchaguliwa  kuwa  waziri  mkuu  wa  jimbo  Juni 27  katika  bunge , Landtag, mrithi  wa  Hannelore Kraft  kutoka chama  cha  siasa  za  wastani  za  mrengo  wa  kushoto Social Democrats , SPD.

NEU Düsseldorf Hannelore Kraft nach Landtagswahl
Hannelore Kraft aliyekuwa kutoka chama cha SPDPicha: Reuters/R. Orlowski

Muungano pamoja  na  chama cha  kijani

Katika  jimbo  la Schleswig-Holstein , jimbo  lililoko kaskazini  kabisa mwa  Ujerumani , chama  cha  CDU  na  FDP vinaelekea  katika kuunda  serikali  pamoja  na  chama  cha  Kijani.

"Tumekuwa  na  mazungumzo  magumu," kiongozi  wa  jimbo  la chama  cha  CDU Daniel Günther  alisema  baada  ya  mazungumzo ya  kuunda  serikali, licha  ya  kuwa  majadiliano  yamekuwa yakifanyika " katika  hali  nzuri  ya maelewano."

Infografik Vorläufiges Ergebnis zur Landtagswahl 2017 in Schleswig-Holstein
Mchoro unaoonesha jinsi chama cha CDU kilivyoshinda katika uchaguzi wa jimbo la Schleswig-Holstein

Mkuu wa  majadiliano  wa  chama  cha  walinzi  wa  mazingira , chama  cha  kijani , Monika Heinold,  amesema  makubaliano yamekuwa  na  kile  alichokiita "alama za  walinzi  wa  mazingira." Kiongozi  wa  FDP Heiner Garg  wakati  huo  huo  alisema  vyama hivyo  vimefanikiwa  katika  kuweka  muongozo  wa "maono  ya baadaye  kwa  ajili  ya  jimbo  hilo  la  Schleswig-Holstein." Msemaji wa   chama cha  FDP  amethibitisha  kwamba  makubaliano yamefikiwa , lakini  hakutoa  maelezo  zaidi.

Kama  ilivyokuwa  katika  jimbo  la  North Rhine Westphalia , chama cha  CDU kiliiondoa  serikali  iliyokuwapo  ambayo  ilikuwa inaongozwa  na  chama  cha  SPD  na  ikijumuisha  chama  cha kijani.

Deutschland Martin Schulz Wahlen Schleswig-Holstein
Mgombea wa ukansela kwa chama cha SPD kitaifa martin SchulzPicha: picture alliance/AP Photo/dpa/M. Schreiber

Merkel  anawania  muhula  wa  nne  madarakani,  amekuwa akiongoza  serikali  ya  mseto  tangu  mwaka  2013  pamoja  na chama  cha  Social Democrats  katika  kiwango  cha  serikali  kuu ya  shirikisho. Chama  cha  Christian Democratic  na  Free Democrats  viliongoza  serikali  ya  Ujerumani  kuanzia  mwaka  2009 hadi  mwaka 2013.

Uchunguzi  wa  maoni  kwa  hivi  sasa  unakipa chama  cha kihafidhina  uongozi  katika  kiwango  cha  kitaifa  kabla  ya  uchaguzi wa  mwezi Septemba, ambapo mgombea  wa  chama  cha  SPD Martin Schulz akipungua  kasi  baada  ya  kupata  uungwaji  mkono mkubwa  mwanzoni.

Mwandishi: Sekione Kitojo /

Mhariri: Yusuf , Saumu