1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha Merkel chakabiliwa na ushindani mkubwa

Caro Robi4 Septemba 2016

Chama kinachowapinga wahamiaji nchini Ujerumani cha Alternative für Deutschland AfD kinatarajiwa kujizolea kura nyingi katika uchaguzi wa jimbo la Mecklenburg West Pomerania leo Jumapili.

https://p.dw.com/p/1JvSd
Picha: picture-alliance/dpa/B. Wüstneck

Uchaguzi huo wa Mecklenburg West Pomerania unaofanyika mwaka mmoja tangu Merkel kuamua kufungua mipaka ya Ujerumani kuwaruhusu mamia kwa maelfu ya wakimbizi kuingia Ujerumani utafuatiwa na uchaguzi mwingine muhimu katika jimbo la Berlin unaotarajiwa wiki mbili zijazo na uchaguzi mkuu unaotarajiwa mwezi Septemba mwakani.

Wapiga kura tayari walimuadhibu Merkel na chama chake cha kihafidhina cha Christian Democartic Union CDU katika chaguzi za majimbo matatu mwezi Machi mwaka huu kwa kukipigia kwa wingi chama cha AfD.

AfD chapata umaarufu mkubwa

Kulingana na kura ya maoni iliyoendesha na shirika la Emnid kwa niaba ya gazeti la Ujerumani la Bild na kuchapishwa Jumapili, iwapo uchaguzi mkuu ungefanyika wiki ijayo, AfD kingeshinda asilimia 12 ya kura na kukifanya chama cha tatu kwa ukubwa nchini Ujerumani. Hiyo inamaanisha kuwa chama hicho kitaingia bungeni kwa mara ya kwanza tangu kilipoundwa mwaka 2013.

Kura ya maoni inayoenyesha wanaomtaka Merkel kuendelea kuwa Kansela wa Ujerumani au la
Kura ya maoni inayoenyesha wanaomtaka Merkel kuendelea kuwa Kansela wa Ujerumani au la

Hapo jana Jumamosi (03.09.2016) Merkel ambaye anatafakari iwapo atagombea Ukansela kwa muhula wa nne katika uchaguzi ujao, aliwaonya wapiga kura wa jimbo la Mecklenburg West Pomerania, dhidi ya kushawishika na siasa zinazoeneza uoga zinazonadiwa na AfD kwa kutumia suala la wakimbizi.

Kansela huyo wa Ujerumani amewahimiza wapiga kura kutizama kupita siasa zinazonuia kuleta migawanyiko na kuzingatia sera za serikali ya sasa ambayo imepunguza ukosefu wa ajira kwa asilimia hamsini na kuimarisha maradufu utalii katika jimbo hilo la pwani anakotokea Merkel.

Katika mahojiano na gazeti la Bild, Merkel ameutetea uamuzi wake wa kuwapokea maelfu ya wahamiaji na wakimbizi wanaotoroka mizozo Mashariki ya Kati na kukanusha kuwa ongezeko hilo kubwa la wakimbizi limesababisha kupunguzwa kwa ufadhili kwa ajili ya raia wa Ujerumani.

Umaarufu wa Merkel umepungua kwa asilimia 45 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita hicho kikiwa kiwango cha chini zaidi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Hata hivyo kiongozi huyo wa Ujerumani amesema atachukua maamuzi kama hayo ya kuwapokea wakimbizi iwapo atakabiliwa na hali kama hiyo hii leo.

Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere ambaye pia ni mwanachama wa chama cha Merkel cha CDU amepinga shutuma kuwa sera ya Merkel kuhusu wakimbizi ndiyo imesababisha kushamiri kwa chama cha AfD.

Je sera ya kuwapokea wakimbizi imemponza Merkel?

Mwanzoni, Merkel alisifiwa sana na kuungwa mkono kwa kuwapokea wakimbizi wanaokimbia vita Syria, Iraq, Afghanistan na kwingineko lakini sifa hizo ziligeuka na kuwa hofu miongoni mwa Wajerumani kuhusu ni namna ipi wakimbizi hao zaidi ya milioni moja watakavyotangamana katika jamii.

Kiongozi wa CSU Horst Seehofer na Kansela Angela Merkel
Kiongozi wa CSU Horst Seehofer na Kansela Angela MerkelPicha: picture-alliance/dpa/R. Hirschberger

Kufuatia misururu ya mashambulizi ya kigaidi iliyodaiwa kufanywa na raia wa kigeni Ujerumani na katika nchi nyingine kama Ufaransa na Ubelgiji, ukarimu kwa wahamiaji na wakimbizi umegeuka kuwa chuki.

Uamuzi huo aliouchukua Merkel umemfanya kutengwa na baadhi ya washirika wake barani Ulaya na kushutumiwa vikali nyumbani hata miongoni mwa wanachama wa chama chake CDU na chama dada Chistian Social Union CSU.

Kura ya maoni iliyotolewa na kituo cha televisheni cha Ujerumani ZDF, ilionyesha AfD itapata asilimia 22 ya kura katika jimbo la Mecklenburg West Pomerania ambalo lina wapiga kura milioni 1.3. CDU pia kilibashiriwa kupata kura sawa na AfD huku chama cha Social Democrats SDP kikitarajiwa kushinda kwa asilimia 28.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/Afp

Mhariri: Sylvia Mwehozi