1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha Netanyahu cha Likud chashinda uchaguzi Israel

18 Machi 2015

Matokeo ya uchaguzi mkuu wa Israel yanaonyesha chama cha Likud kinachoongozwa na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kimeshinda katika uchaguzi huo na hivyo kumhakikishia Netanyahu muhula mwingine madarakani.

https://p.dw.com/p/1EsQl
Picha: Reuters/Amir Cohen

Tume ya uchaguzi nchini Israel imetangaza hii leo kuwa chama cha Likud kimejinyakulia viti thelathini kati ya 120 vya bunge na hivyo kuwa katika nafasi ya kuunda serikali ijayo ya muungano na vyama vya mrengo wa kulia.

Uchaguzi huo wa jana ambao ulikuwa kinyang'anyiro kikali kati ya Netanyahu na mpinzani wake wa karibu Isaac Herzog wa chama cha umoja wa Uzayuni ulionekana kama kura ya maoni kuhusu utawala wa Netanyahu ambaye amekuwa madarakani kwa miaka sita iliyopita.

Herzog akubali kushindwa

Matokeo yanaonyesha chama cha Herzog kimejishindia viti 24 vya bunge. Asilimia 99 ya kura tayari zimeshahesabiwa. Herzog amesema amempigia simu Netanyahu kumpongeza kwa ushindi alioupata na kumtakia kila la kheri. Kura za maoni kabla ya uchaguzi huo zilikuwa zimeonyesha chama cha umoja wa Zayunni kingekishinda cha Likud kwa karibu viti vinne vya bunge.

Mgombea wa chama cha umoja wa Uzayuni Isaac Herzog
Mgombea wa chama cha umoja wa Uzayuni Isaac HerzogPicha: Reuters/B. Ratner

Kurejea madarakani kwa Netanyahu kunabashiriwa kuubakisha uhusiano kati ya Israel na Palestina katika hali ya mkwaruzano na pia kuzidisha hali tete kati yake na Rais wa Marekani Barack Obama kuhusu sera za kigeni.

Katika mkondo wa mwisho wa kampeni, Netanyahu aliapa kutoruhusu kuundwa kwa dola la Palestina, ataendelea kuyajenga makaazi ya walowezi wa kiyahudi katika maeneo yanayozozaniwa na kusema Iran inasalia kuwa kitisho kikubwa kwa usalama na uthabiti wa Israel, ahadi ambazo zinaaminika ndizo zilizowashawishi wapiga kura.

Serikali mpya kuundwa majuma machache yajayo

Taarifa kutoka chama cha Likud imesema Netanyahu ananuia kuunda serikali katika kipindi cha wiki chache zijazo huku mazungumzo yakiwa yameshaanza na kiongozi wa chama kinachowaunga mkono walowezi wa kiyahudi Naftali Bennet pamoja na makundi ya kidini. Netanyahu amesema mchakato huo haupaswi kuchelewa.

Wafuasi wa chama cha Likud wakisherehekea mjini Tel Aviv
Wafuasi wa chama cha Likud wakisherehekea mjini Tel AvivPicha: Reuters/A. Cohen

Mgombea wa chama cha Kulanu, Moshe Kahlon ambaye chama chake kimeshinda viti kumi vya bunge anaoekana mshirika muhimu katika kuunda serikali ijayo ya mseto kutokana na uwezo wake wa idadi ya viti alivyovipata kwa kuamua kumuunga mkono Netanyahu au upande wa vyama vya msimamo wa wastani vya mrengo wa kushoto.

Iwapo Netanyahu ataweza kuunda serikali ya mseto, itampa muhula wa nne madarakani na hivyo kumfanya kuwa waziri mkuu wa kwanza Israel kuhudumu kwa muda mrefu zaidi na kumpiku muasisi wa taifa hilo David Ben Gurion.

Licha ya kuwa Likud ndicho chama kikubwa zaidi cha kisiasa, mchakato wa kuunda serikali ya mseto huenda ikawa safari ngumu. Inahitaji viti sitini na vimoja bungeni na kufikia hilo ni changamoto kubwa kutokana migawanyiko iliyoko katika siasa za Israel.

Mkuu wa ujumbe wa wapatanishi wa Palestina katika mazungumzo ya kutafuta amani na Israel Saeb Erekat amesema ni bayana Netanyahu ataunda serikali ijayo na kuongeza muda wote ambao Netanyahu amekuwa madarakani hajafanya jingine ila kuvunja juhudi za kupatikana suluhisho la kuwa na mataifa mawili.

Mwandishi:Caro Robi/Reuters/Ap

Mhariri: Grace Patricia Kabogo