1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha upinzani Zimbabwe chalalamikia mkwamo wa kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa

Mohamed Dahman8 Oktoba 2008

Chama cha upinzani nchini Zimbabwe cha MDC kimeelezea masikitiko yake kwamba kimesaini makubaliano ya kushirikiana madaraka bila ya kwanza kukubaliana juu ya muundo wa serikali ya umoja wa kitaifa.

https://p.dw.com/p/FWBw
Mashabiki wa chama kikuu cha upinzani MDC nchini Zimbabwe.Picha: AP

Akizungumza katika radio ya Afrika Kusini juu ya kucheleweshwa kwa wiki tatu utekelezaji wa makubaliano hayo ya kihistoria msemaji wa chama cha MDC Nelson Chamisa amesema anadhani kosa kubwa la chama hicho ni kule kusaini makubaliano hayo kabla ya kukamilishwa kwa mazungumzo.

Matumaini ya kukomesha mgogoro wa kiuchumi na wa kisiasa nchini Zimbabwe yalikuwa makubwa wakati Rais Robert Mugabe aliposaini makubaliano hapo Septemba 15 kushirikiana madaraka na mpinzani wake wa muda mrefu Morgan Tsvangirai.

Chini ya makubaliano hayo yaliosuluhishwa na Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini Mugabe anaendelea kubakia kuwa rais wakati madaraka yake yakipunguzwa na Tsvangirai anakuwa waziri mkuu.

Wiki tatu baadae hofu kwamba makubaliano hayo yanaweza kusambaratika zimekuwa zikiongezeka wakati chama cha ZANU- PF cha Mugabe na kile cha MDC vinaendelea kuzozana juu ya namna ya kugawana nyadhifa za mawaziri baina yao.

Kiongozi wa chama tawala cha Afrika Kusini Jacob Zuma hapo jana amezihimiza pande hizo mbili kusonga mbele kutimiza makubaliano hayo.

Akionekana kutozipa uzito habari za nyadhdifa za mawaziri Zuma amesema wameweza kutatuwa masuala mengi magumu.

Makubaliano hayo ya kugawana madaraka yametaja tu kijujuu kwamba ZANU-PF itakuwa na nyadhifa 15 za mawaziri,MDC itakuwa na 13 na kundi dogo lililojitenga na MDC linaloongozwa na Arthur Mutambara litakuwa na nyadhifa tatu za mawaziri.

Katika suala la kugawana nyadhifa za mawaziri chama cha ZANU-PF kimesema mwishoni mwa juma kwamba mzozo huo sasa uko katika wizara za fedha na mambo ya ndani wakati chama cha MDC kinatupilia mbali madai hayo kwamba ni nyadhifa mbili tu zinazogombaniwa na kimesema kwamba wamekwama katika suala la kugawana nyadhifa zote muhimu za mawaziri na magavana.

Chama hicho kimetaka msaada kutoka Jumuiya ya Ushirikiano wa Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika SADC na Umoja wa Afrika.

Chama cha MDC kinasema kwamba nchi hiyo iko kwenye mkwamo na subira ya watu inayoyoma na ndio sababu ufumbuzi wa mkwamo huo ni wa dharura zaidi kuliko ilivyokuwa kabla.

Afisa mwandamizi wa ZANU-PF amesema mapema wiki kwamba Mugabe alikuwa akitegemewa kukutana na kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai katika siku mbili hizi katika jaribio jengine la kuondowa kikwazo juu ya nyadhifa hizo za mawaziri.

Bila ya kupatikana ufumbuzi uchumi wa Zimbabwe unaweza kuathirika zaidi.Taifa hilo ambalo huko nyuma lilikuwa likistawi linasambaratika kutokana na kupanda kwa gharama za maisha za takriban asilimia milioni 11 ambacho ni kiwango kikubwa kabisa duniani na pia tatizo la uhaba wa chakula limekuwa sugu.

Baadhi ya wanauchumi wanaamini kwamba kiwango cha kupanda kwa gharama za maisha nchini Zimbabwe hivi sasa kimepindukia asilimia milioni 40.

Serikali za mataifa ya magharibi zimekuwa zikisubiri kuingiza mamlioni ya dola za msaada na uwekezaji nchini Zimbabwe iwapo kutakuwepo na serikali itakoyohodhiwa na chama cha MDC.