1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Champions League

Ramadhan Ali3 Oktoba 2007

Kombe la klabu bingwa la Ulaya larudi uwanjani leo huku mabingwa Ac Milan wakitetea taji lao.Kesho ni zamu ya kombe la UEFA.

https://p.dw.com/p/CHat
AC Milan itaweza kutetea kombo hilo zuri?
AC Milan itaweza kutetea kombo hilo zuri?Picha: AP

Champions League-kombe la klabu bingwa barani Ulaya laendelea jioni hii baada ya jana mabingwa wa Ujerumani Stuttgart kuzabwa mabao 2:o nyumbani na FC Barcelona ya Spain na Manchester united kuilaza AS Roma ya Itali kwa bao la 1 la Wayne Rooney. Leo mabingwa watetezi AC Milan ya Itali wanarudi uwanjani kutetea taji lao huku macho yakikodolewa Chelsea.

Mabingwa watetezi wa champions League-AC Milan ya Itali wanabidi nao kusahau misukosuko ya nyumbani ya serie A wanapokumbana leo na Celtic Glasgow.

Milan imekuwa ikipepesuka nyumbani na hiyo si ishara njema kwa changamoto za kombe hili la klabu bingwa barani Ulaya.

Nahodha wa Uingereza John Terry,atazamiwa leo kuiongoza Chelsea –mabingwa mara 2 wa Uingereza katika mpambano wao leo na Valencia ya Spain.Kucheza leo kwa Terry kutawatia moyo sana Chelsea ambayo haikushinda mechi yoyote mwezi sasa katika premier League-ligi ya Uingereza.

Katika mpambano wao wa kwanza wa champions League, Chelsea kinyume na wenzao Manchester, walimudu suluhu tu ya bao 1:1 na chipukizi Rosenborg.Kocha mpya Grant aliechukua kiti cha Jose Mourinho,anajua mpambano wa leo kwa Chelsea huenda ukaamua na mapema hatima yake.

Jana mabingwa wa Ujerumani VFB stuttgart walishindwa kutamba nyumbani mbele ya FC Barcelona ya Spain ikicheza na Ronaldinho wa Brazil na Lionel Messi wa argentina.Barcelona iliondoka na ushindi wa mabao 2:0 huko Stuttgart.

Vishindo vya Mario Gomez katika lango la Barcelona havikufua dafu kwani, Carles Puyol na mwenzake Lionel Messi, walinasa mabao 2 katika wavu wa Stuttgart.Mabao yote 2 yametokana na madhambi ya walinzi wa mabingwa wa Ujerumani.

Wakati stuttgart imeteleza.Manchester united haikujionea neema ya magoli mbele ya AS Roma kama msimu uliopita, lakini bao la Wayne Rooney,lilitosha jana kuwarejesha Roma nyumbani Itali mikono mitupu. Arsenal pia ilitamba kama MANU .

Bao la Robin van Persie liliipa Arsenal ushindi wa bao1 dhidi ya Steaua Bucharest ya Romania hapo jana.Pasi maridadi kutoka kwa Mtogo Emmanuel Adebayor, lilimkuta Robin pekee akilifumania lango la Bucharest.

Kesho ni zamu ya kombe la Ulaya la UEFA na viongozi wa Ligi wa Ujerumani, Bayern Munich watabidi kucheza na Belenenses ya ureno bila kipa Oliver Kahn na wala bila mshambulizi Miroslav Klose.Kuna shaka shaka pia iwapo mholanzi Mark van bommel au Bastian schweinsteiger watacheza.

Bayer Leverkusen inateremka duru ya kwanza ya kombe hili ikicheza pia kesho na timu nyengine ya Ureno-Leiria nayo pia bila ya mtiaji wao magoli mgiriki Thofanis Gekas.Timu zote 2 za ujerumani hatahivyo, zatumai kuwika.

Kesho Bayern munich na Bayer Leverkusen kuteremka nazo uwanjani kwa kombe la Ulaya la UEFA.Munich bila jogoo lao Miroslav Klose na kipa Oliver Kahn.