1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Changamoto ya vikosi vya kulinda amani

P.Martin7 Novemba 2006

Umoja wa Mataifa unajitayarisha kuongeza idadi ya wanajeshi wake wa kulinda amani duniani kutoka 93,000 ya hivi sasa kufikia hadi 140,000 hapo mwakani.

https://p.dw.com/p/CHLF

Mbali na Marekani,idadi kubwa kabisa ya vikosi vilivyotawanywa sehemu mbali mbali duniani ni vya Umoja wa Mataifa.Katibu Mkuu wa Umoja huo,Kofi Annan amesema,aliposhika madaraka hayo miaka kumi ya nyuma,Umoja wa Mataifa ulikuwa na wanajeshi wa amani 20,000 kazini.Sasa akikaribia kuacha wadhifa huo mwezi wa Desemba,idadi ya vikosi vya amani vya umoja huo vimefikia kiwango cha juu kabisa katika historia yake.

Kufuatia maazimio ya hivi karibuni ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa,kuongeza vikosi nchini Lebanon na Timor ya Mashariki,jumla ya wanajeshi 112,000 wanashiriki katika operesheni 18 za Umoja wa Mataifa kote duniani.

Ikiwa Sudan,baadae itakubali kuviruhusu vikosi vipya vya amani katika jimbo la Darfur licha ya upinzani wake wa hivi sasa,basi idadi ya wanajeshi wa Umoja wa Mataifa itapindukia 140,000.

Katibu Mkuu Kofi Annan alipotoa hotuba ya kuadhimishwa mwaka wa 50 tangu kuundwa kikosi cha kwanza cha amani cha umoja huo yaani Kikosi cha Dharura katika Mashariki ya Kati-UNEF-alisema, sasa,baada ya kuwa na tume 60,operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa zimekuwa silaha muhimu katika ghala ya silaha za jumuiya ya kimataifa.Operesheni hizo zinatoa nafasi ya kuchukua hatua kwa njia ya kisheria na bila ya upendeleo migogoro inapozuka:hutoa nafasi ya kusaidiana kubeba mzigo:pia ni njia inayofaa kuchukua hatua dhahiri na ni daraja la kuleta utulivu na amani ya kudumu na maendeleo.

Wakati huo huo Annan alionya kuwa vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa vinakabiliwa na changamoto nyingine kubwa.Akaeleza kuwa vikosi vya umoja huo vina operesheni nyingi kuliko hapo zamani.Juu ya hivyo changamoto hiyo inakabiliwa kwa matumaini.

Kutoka jumla ya operesheni hizo 18 za Umoja wa Mataifa,8 zinashughulika barani Afrika. yaani Sahara ya Magharibi,Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,Ethiopia na Eritrea,Liberia,Ivory Coast, Burundi,Sudan na Sierra Leone.Idadi kubwa kabisa ya vikosi hutoka nchi zinazoendelea.Nchi kumi zinazoongoza ni Bangladesh,Pakistan,India,Jordan, Nepal,Ethiopia,Ghana,Nigeria,Uruguay na Afrika ya Kusini.

Hivi sasa asili mia 67 ya watumishi wa kijeshi na polisi wa Umoja wa Mataifa hutoka nchi zinazoendelea na chini ya asili mia 5.8 hutoka nchi za Umoja wa Ulaya na asili mia 0.5 ni kutoka Marekani.

Tume za kulinda amani za Umoja wa Mataifa zinaundwa na kupangwa na Baraza la Usalama lenye wanachama 15,miongoni mwao 5 wakiwa wanachama wa kudumu wenye usemi mkubwa.Nchi hizo ni Marekani, Uingereza,Ufaransa,China na Urussi.

Akitoa mwito wa kulipanua Baraza la Usalama- mpango unaojadiliwa kwa zaidi ya miaka 20-Annan amesema,haitokuwa rahisi kuongeza idadi ya vikosi kutoka nchi zinazohisi kuwa haziwakilishwi vya kutosha katika Baraza la Usalama linaloamua juu ya mamlaka ya tume za kulinda amani.