1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Changamoto za kuijenga upya Libya

24 Agosti 2011

Mapigano makali yakiendelea katika mji mkuu wa Libya Tripoli, wanadiplomasia na wakuu wa taasisi za fedha wanaharakisha miradi ya kuwasaidia Walibya kuijenga upya nchi yao, baada ya enzi ya Gadaffi kumalizika.

https://p.dw.com/p/Rhn9
epa02648971 (FILES) A file photo taken 10 March 2011 showing Mahmoud Jibril of the Libyan National Transitional Council arriving at the Elysee Palace for talks with French President Nicolas Sarkozy. It was announced 23 March 2011 that he has been elected the 'leader of the Libyan rebels in Benghazi', according to Arabian tv reports. EPA/MAXPPP/CHRISTOPHE MORIN FRANCE OUT - BELGIUM OUT +++(c) dpa - Bildfunk+++
Waziri Mkuu wa Baraza la Mpito la Kimataifa Libya, Mahmoud JibrilPicha: picture-alliance/dpa

Libya yenye utajiri mkubwa wa mafuta inakabiliwa na changamoto kali za kisiasa na kiuchumi, nchi hiyo ikijaribu kujitoa kutoka utawala wa kidikteta wa miongo minne. Baraza la Mpito la Kitaifa NTC, linaloongozwa na waasi wa Libya, limetayarisha mpango wa kurejesha utulivu upesi iwezekanavyo. Baraza hilo halina budi kufanya hivyo, ili kutimiza matumaini ya umma uliosaidia kumaliza utawala wa Muammar Gadaffi baada ya miaka 42. Wasiwasi mkubwa wa NTC ni kwamba Marekani na mataifa mengine yaliyozuia mali ya Gadaffi yenye thamani ya mabilioni ya dola, yatakawia kuziachia fedha hizo na hiyo itaathiri vibaya huduma za kijamii nchini Libya. Kwa hivyo, kama njia ya mpito, baraza hilo linazingatia kuomba msaada wa dola bilioni 2.5 kutoka Benki ya Dunia na taasisi zingine za kimataifa, mpaka mali yote ya Libya itakaporejeshwa.

Waziri Mkuu wa NTC, Mahmoud Jibril hii leo alisema, wanachama wa baraza hilo wanakutana na waakilishi wa Marekani, Ufaransa, Italia, Uingereza, Uturuki na Qatar mjini Doha, kulijadili suala hilo. Alipozungumza na waandishi wa habari katika mji mkuu wa Qatar, Doha, Jibril alisema sasa ni wakati wa kusahau yaliyopita na kuijenga upya nchi yao. Ni matumaini yake kuwa msaada wa fedha utapatikana kabla ya mwezi huu mtukufu wa Ramadhan kumalizika, ili Walibya wapate kulipwa mishahara yao na majeruhi kupewa matibabu. Amesema, kipaumbele ni kupata fedha zilizozuiliwa na kuanzisha upya shughuli za uchimbuaji wa mafuta, upesi iwezekanavyo.

Fire and flares go up after several large explosions went off in the capital city of Tripoli, Libya, early Sunday, Aug. 7, 2011. Several large explosions rocked the city and fires could be seen in the distance. (Foto:Dario Lopez-Mills/AP/dapd)
Miripuko iliyoutikisa mji mkuu TripoliPicha: dapd

Umoja wa Ulaya na Marekani zinajiandaa kuachilia mali ya Libya iliyozuiliwa, ikiwa na thamani ya mabilioni ya dola. Hapo jana, Umoja wa Ulaya uliarifu kuwa unafanya matayarisho ya kuziachia fedha hizo, baada ya kupata idhini ya Umoja wa Mataifa. Hata Rais wa Marekani Barack Obama amesema, yeye yupo tayari kuchukua hatua kama hiyo. Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani, hizo na kiasi cha dola bilioni 1 na bilioni 1.5 kutoka jumla ya dola bilioni 32 zilizozuiliwa na Marekani mapema mwaka huu.

China ilio na uwekezaji mkubwa nchini Libya imesema, inatazamia kuwa na dhima muhimu katika kuijenga upya Libya, kwa kushirikiana na jumuiya ya kimataifa. Hayo alitamka, msemaji wa wizara ya biashara ya China, Shen Danyang hii leo mjini Beijing. Amesema, serikali yo yote itakayokuwa madarakani Libya inapaswa kuzingatia mahitaji ya masoko na masalahi ya kiuchumi. Matamshi hayo yanafuatia mwito wa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa China, Yeng Jiechi kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa hapo jana, kuwa umoja huo ndio uratibu miradi ya kimataifa katika taifa jipya la Libya, badala ya serikali za magharibi pekee.

Mwandishi: Martin,Prema/rtre/afpe

Mhariri: Abdul-Rahman, Mohammed