1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Changamoto za serikali mpya ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya17 Desemba 2013

Serikali mpya ya mseto wa vyama vikuu inatarajiwa kuanza kazi, wakati ambapo mifuko imejaa vizuri. Hata hivyo serikali hiyo itakabiliwa na changamoto kubwa na hasa katika sekta ya nishati.

https://p.dw.com/p/1Aauh
Kansela Angela Merkel apitishwa na bunge kuutumikia muhula wa tatu
Kansela Angela Merkel apitishwa na bunge kuutumikia muhula wa tatuPicha: Reuters

Kansela Angela Merkel hana haja ya kulalamika juu ya hali iliyopo sasa nchini Ujerumani. Uchumi wa nchi ni mzuri kuliko wa nchi yoyote nyingine barani Ulaya. Serikali ya mseto ya vyama vya CDU,SPD na CSU itaweza kutumia fedha nyingi tu. Hata hivyo fedha nyingi peke yake hazitaikatua ngwe yote.

Jukumu kubwa kabisa linalotarajiwa kuikabili serikali mpya ya Ujerumani ni kuleta mageuzi katika sekta ya nishati Mradi huo wa kuleta mageuzi umeanzishwa kwa kishindo kikubwa baada ya Kansela kuamua kuyaleta mageuzi hayo kutokana na maafa ya kinyuklia yaliyotukia Fukushima nchini Japan.

Ujerumani inakusudia kuondokana na matumizi ya nishati ya nyuklia hadi kufikia mwaka wa 2020. Nishati mbadala, za upepo, nguvu jua na maji zitachukua mahala pa nishati ya nyuklia.Lakini mradi huo umekwama.

Majukumu ya Waziri Sigmar Gabriel

Mwenyekiti wa chama cha Social Demokratik Sigmar Gabriel ambaye sasa ni Waziri wa uchumi, pia atayasimamia masuala ya nishati.

Mshauri wa masuala ya kisiasa Michael Spreng amesema hiyo ni fursa kwa Waziri Gabriel, lakini wakati huo huo ni changamoto kubwa inayoandamana na mashaka. Mshauri huyo ametilia maanani kwamba Waziri Gabriel ambae pia ni makamu wa Kansela atahitaji kuwa na nguvu kama ndovu ili kuweza kulitekeleza jukumu linalomkabili. Lakini mshauri huyo pia amezungumzia juu ya gharama kubwa za mradi huo zinazoweza kutoa ishara mbaya kwa nchi nyingine barani Ulaya.

Amesema kwa mradi huo serikali mpya inatoa ishara mbaya. Nchi nyingine barani Ulaya zitashangazwa kuona kwamba katika upande mmoja Ujerumani inahubiri sera ya kubana matumizi lakini katika upande mwingine inamwaga fedha kwa ajili ya mradi wa nishati." Mshauri huyo wa masuala ya kisiasa Michael Spreng amesema mpaka sasa maswali muhimu bado hayajajibiwa: kwa mfano, jee bei za gesi na nishati ya umeme zitaweza kulipika,na jee nini kitatokea kwa nishati ya makaa ya mawe inayoharibu mazingira na vipi mtandao wa ugavi wa nishati ya umeme utaweza kujengwa kwa haraka?

Andrea Nahles

Waziri mwingine kutoka chama kikuu cha upinzani SPD Andrea Nahles atakaeiongoza wizara ya kazi ataitekeleza ahadi ya kuanzisha utaratibu wa mshahara wa wastani wa kima cha chini wa Euro 8 ,50 kwa saa.Mambo yamekaa vizuri kwa Waziri huyo na hivyo ataweza kuchukua hatua nyingine za kuleta ustawi wa kijamii, moja wapo ni kuwawezesha wafanya kazi kustaafu wakiwa na umri wa miaka 63 na kupata malipo kamili.

Changamoto ya Afghanistan

Wazri mpya wa ulinzi Ursula von der Leyen kutoka chama cha CDU pia atakuwa na mzigo wake wa kuubeba na hasa kuhusiana na suala la Afghanistan.Kwa mfano nini kitatokea kwa wafanyakazi wananchi wa Afghanistan ambao wamekuwa wanalisaidia jeshi la Ujerumani nchini Afghanistan.Watu hao wanatishiwa na mataliban.Na karibu wote wameomba hifadhi nchini Ujerumani?

Mwandishi: Siffert Jeanette

Tafisri:Mtullya Abdu.

Mhariri:Yusuf Saumu