1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Changamoto za Umoja wa Ulaya zajadiliwa Brussels

15 Desemba 2016

Mkutano wa Umoja wa Ulaya ambapo viongozi 27 wanatarajiwa kuafikia makubaliano kuhusu mazungumzo ya kujiondoa kwa Uingereza katika Umoja huo ulizua hali ya kutoelewana pale wabunge walipotaka jukumu kubwa zaidi

https://p.dw.com/p/2UJwZ
Symbolbild EU
Picha: Getty Images/AFP/E. Dunand

Ijapokuwa bunge la Umoja wa Ulaya litabidi kuidhinisha hatua yoyote ya kujiondoa kwa Uingereza katika muungano huo baada ya mazungumzo hayo, mataifa ya Umoja huo yanapanga kumteuwa Michel Barnier kuwa mpatanishi mkuu na kuliachia bunge hilo kutekeleza jukumu dogo.
Katika pendekezo la bunge hilo lililoonekana na shirika la habari la Associated Press, wabunge hao wanataka kuhudhuria vikao vyote vya mazungumzo hayo. Afisa mkuu wa bunge hilo katika mazungumzo hayo Guy Verhofstadt, ametishia kuanzisha mazungumzo sambamba na Uingereza.
Verhofstadt aliongeza kuwa iwapo baraza hilo halitalitaka bunge hilo katika chumba hicho cha mazungumzo basi litaanzisha mashauriano moja kwa moja na Uingereza.

May atoa wito wa mpangilio katika kujiondoa kwa Uingereza 

Wakati huo huo, waziri mkuu wa Uingereza Theresa May amewahimiza wenzake katika Umoja wa Ulaya kuhakikisha kuwa hatua ya Uingereza ya kujitoa katika Umoja huo inatekelezwa kwa njia shwari huku wanapojiandaa kulijadili suala hilo hii leo katika dhifa ya jioni ambayo hatahudhuria. 
Mbali na suala hilo la kujiondoa kwa Uingereza katika Umoja huo, Rais wa Ufaransa Francois Hollande alisema  anawataka viongozi katika mkutano huo kutoa wito wa kusitishwa kwa mashambulizi mjini Aleppo kuwawezesha raia na majeruhi kuhamishwa kutoka eneo hilo.
Akitaja mpango wa kuhakikisha usalama katika mji huo nchini Syria, aliwaambia waandishi habari kuwa kwa haya yote kuwezekana, pendekezo la kusitishwa kwa mashambulizi lazima litekelezwe na huu ndio wito unaopaswa kutolewa na Umoja wa Ulaya.
Rais wa Umoja  wa Ulaya Donald Tusk anatarajiwa kukutana na meya wa Aleppo Brita Hagi Hassan aliye mjini Brussels kushinikiza Umoja huo kuunga mkono kufunguliwa kwa njia ya mashirika ya misaada ya kibinadamu kuwahamisha raia kutoka eneo hilo.
Viongozi hao watatoa taarifa kwamba Umoja wa Ulaya unashtumu vikali mashambulizi yanayotekelezwa na serikali ya Syria na washirika wao Urusi na kusema kuwa Umoja huo unakadiria njia zote zilizoko kulingana na rasimu iliyoonekana na shirika la habari la AFP.
Mkutano huo pia unalenga kuangazia masuala mengine kama vile kukabiliana na uhamiaji kutoka Afrika na kuimarisha ulinzi dhidi ya Urusi huku Donald Trump akijitayarisha kuchukuwa uongozi wa Marekani, agenda inayowatia hofu Waingereza wengi kwamba huenda ikatatiza hatua ya Marekani ya kujitolea kuwalinda dhidi ya Urusi.

Belgien EU Gipfel Theresa May
Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May awasili katika mkutano wa Umoja wa Ulaya mjini BrusselsPicha: picture-alliance/AP Photo/V. Mayo

Mwandishi: Tatu Karema/afpe/reuters
Mhariri:Yusuf Saumu