1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chanzo cha mashambulio ya Mumbai hakijajuilikana

14 Julai 2011

Waziri wa Mambo ya Ndani wa India amesema polisi bado hawajapata taarifa za haraka juu ya chanzo cha mashambulio ya mabomu yaliyotokea kwenye mji wa Mumbai jana usiku, wakati ambapo mji huo, uko katika tahadhari ya juu.

https://p.dw.com/p/11v1L
Vikosi vya jeshi vikiwa katika Ulinzi wa hali ya juuPicha: dapd

Waziri wa Mambo ya Ndani wa India Palaniappan Chidambaram ambaye alitembelea maeneo ambayo milipuko hiyo mitatu ilitokea katika mji huo mkuu wa kibiashara nchini humo, aliarifu pia kuongezeka kwa idadi ya watu waliokufa katika shambulio hilo na kufikia 18. Amesema watu wengine 131 wamejeruhiwa katika mashambulio hayo aliyoyaita ya "kupangwa", huku watu 23 wakiwa katika hali mbaya.

Indien Mumbai Terroranschlag
Watu wakiwa wametaharukiPicha: dapd

Amesema wamekuwa wakiyashuku makundi yote makubwa ambayo yanauwezo wa kufanya mashambulio kama hayo ya kigaidi. Lakini hata hivyo amesema hawatalinyooshea kidole kundi lolote lile kabla ya kumalizika kwa uchunguzi, na kufahamisha kuwa uchunguzi ulianza mara moja baada ya mashambulio hayo, jana usiku.

Amesema "..makundi yote yenye uadui na India yapo kwenye hesabu yetu, hatupuuzii chochote wala hatutii chumvi chochote tutamtafuta kila mtu na tutagundua aliyehusika na mashambuzi haya..''.

Hata hivyo alikanusha taarifa kwamba ushahidi muhimu utakaotumika mahakamani dhidi ya shambulio hilo umefutika, kutokana na mvua nyingi za msimu zinazonyesha.

Hata hivyo alipoulizwa kwamba shambulio hilo litaathiri mazungumzo yajayo ya amani kati ya India na Pakistan, iwapo makundi ya wapiganaji ya Pakistan yatatiwa hatiani, Waziri wa Mambo ya Ndani wa India alijibu kuwa makundi yote yanayojulikana wanachunguzwa. huku akiongezea kusema wako jirani na nchi zenye kujulikana na masuala ya kigaidi duniani, Pakistan na Afghanistan.

Mpaka sasa hakuna kundi lolote la kigaidi lililodai kuhusika na mashambulio hayo yaliyotokea katika mji wa Zaveri Bazar na pia katika eneo la Dadar. Mashambulio hayo yalitokea jana jioni muda ambao watu wako katika pilika pilika nyingi.

Kwa upande wake Kamanda wa polisi katika mji huo, Singh Bhati, akifafanua zaidi jinsi uchunguzi huo utakavyofanyika.

Indien Mumbai Terroranschlag
Uharibifu mkubwaPicha: dapd

Amesema watafanya ukaguzi hususan kwenye mahoteli na katika nyumba za kulala wageni, na pia barabarani kwa vitu wanavyotilia wasiwasi, magari au hata watu.

Milipuko yote mitatu ilitokea katika kipindi cha dakika 15 ambapo magari na pikipiki zilitumika katika mashambulio hayo.

Shambulio hilo ni kubwa kuua watu wengi nchini humo, tangu lile lililotokea mwaka 2008 baada ya wapiganaji 10 wa Kipakistan kushambulia maeneo kadhaa katika mji huo na kuua watu 166, na wengi 244 walijeruhiwa.

Mwandishi: Halima Nyanza(dpa, afp, al Jazeera)

Mhariri: Abdul-Rahman,Mohammed