1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chelsea, Real Madrid zafuzu, BVB, PSG zaumia

Admin.WagnerD9 Aprili 2014

Chelsea ilifanikiwa kugeuza nakisi ya magoli mawili dhidi ya Paris Saint-Germain Jumanne usiku, huku Real Madrid nayo ikisonga mbele katika hatua ya nusu fainali ya klabu bingwa barani Ulaya.

https://p.dw.com/p/1Be8B
Borrusia Dortmund wakimenyana na Real Madrid.
Borrusia Dortmund wakimenyana na Real Madrid.Picha: picture-alliance/dpa

Mzaliwa wa mji wa Paris Demba Ba alifunga dhidi ya klabu ya mji wake wa nyumbani PSG, katika ushindi wa magoli mawili kwa bila katika uwanja wa Stamford Bridge na kuipeleka Chelsea katika nusu fainali chini ya sheria ya magoli ya ugenini.

Baada ya kipigo cha magoli matatu kwa moja mjini Paris wiki iliyopita, winga wa Ujerumani Andrea Schuerrle ndiye alianza kurejesha matumaini ya Chelsea katika duru ya pili kwa mkwaju wa kipindi cha kwanza.

Lakini alikuwa mchezaji wa Akiba Demba Ba alieipachika goli muhimu katika dakika ya 87 na kuyafanya matokeo kuwa matatu kwa matatu.

Paris Saint-Germain walishindwa kutetea ushindi wao wa magoli 3-1 dhidi ya Chelsea na hivyo kunagukia pua.
Paris Saint-Germain walishindwa kutetea ushindi wao wa magoli 3-1 dhidi ya Chelsea na hivyo kunagukia pua.Picha: Reuters

Madrid yafuzu licha ya kipigo

Wakati ushindi wa duru ya kwanza haukutosha kwa PSG, hali ilikuwa tofauti kwa Real Madrid, ambao walitinga katika nusu fainali yao ya nne mufululizo kwa jumla ya magoli matatu kwa mawili licha ya kipigo cha magoli mawili kwa sifuri nyumbani kwa Borrusia Dortmund.

Wakati Chelsea ikibakia kwenye mkondo wa kushinda taji la klabu bingwa kwa mara ya pili katika misimu mitatu, klabu ya zamani ya Mourinho Madrid nayo pia iko katika nne bora, hatua ambayo wamekuwa wakiifikia lakini wakashindwa kuivuka katika kila mmoja ya miaka mitatu ya Mreno huyo aliyokaa katika uwanja wa Bernabue.

Mabingwa hao wa Uhispania walifanikiwa kusonga mbele, shukurani kwa ushindi wao wa magoli 3-0 katika duru ya kwanza wiki iliyopita, ingawa walipata kibano cha kutisha katika uwanja wa Westfalenstadion.

Christiano Ronaldo alikaa benchi kipindi chote cha mchezo kutokana na tatizo la goti, na Penati ya Angel Di Maria iliokolewa na mlinda mlango wa Dortmund Roman Weidenfeller, kabla ya Marco Reus kutumia makosa ya wachezaji wa Real Madrid Pepe na kufunga magoli mawili katika kipindi cha kwanza.

MAnchester United kutupa karata yake dhidi ya mabingwa watetezi Bayern Munich Jumatano usiku.
MAnchester United kutupa karata yake dhidi ya mabingwa watetezi Bayern Munich Jumatano usiku.Picha: Getty Images/Alex Livesey

Dortmund walianza kuhisi wanaweza kugeuza kipigo cha duru ya kwanza, lakini hawakufanikiwa kusawazisha mechi hii kwa jumla ya magoli, huku Henrikh Mkhitaryan akikaribia alipomzungusha Casillas, lakini mkwaju wake ukagonga mwamba katika dakika ya 65.

Ngwe ya pili

Orodha ya timu zitakazocheza nusu fainali itakamilika hii leo wakati Atletico Madrid itakapoikaribisha Barcelona, na Bayern Munich inachuana na Manchester United, huku timu zote zikiwa zilifungana gaoli moja kwa moja.

Kwa PSG, ni msimu mwingine wa kuvunja moyo katika robo fainali, baada ya kuwa mhanga wa sheria ya magoli ya ugenini, kama ilivyokuwa kwa Barcelona mwaka uliyopita.

Ingawa subira ya PSG ya kuingia hatua ya nusu fainali itaingia mwaka wake wa 20, timu hiyo iko mbioni kutetea taji lake la Ligi kuu ya Ufaransa, ikiwa inaongoza kwa tofauti ya alama 13.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,ape

Mhariri: Charo Josephat