1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cheney Ziarani Iraq,mashambulio yakizidi nchini humo

9 Mei 2007

Makamu war ais amefanya ziara ya ghafla mjini Baghdad hii leo kwa lengo la kukutana na waziri mkuu wa nchi hiyo Nuri Al Maliki miongoni mwa mambo mengine.

https://p.dw.com/p/CB4D
Makamu wa rais wa Marekani Dick Cheney
Makamu wa rais wa Marekani Dick CheneyPicha: AP

Makamu war ais wa Marekani Dick Cheney yuko mjini Baghdad kwa ziara yake ya ghafla kwa lengo la kukutana na viongozi wa nchi hiyo inayoendelea kukabiliwa na kitisho cha mauaji ya kimadhehebu.

Bwana Cheney anatarajiwa kuwataka viongozi wa Iraq kuongeza nguvu juhudi zao za kuleta maridhiano na vile vile kuwaonya kwamba subira ya Marekani inazidi kupotea.

Akikutana na balozi wa Marekani nchini Iraq Ryan Crocker na kamanda mkuu wa jeshi la Marekani nchin i Iraq Generali David Patraeus alisema na hapa tunanukulu.

Kuna mengi yanayoendelea,huu ni wakati muhimu kabisa kuna mengi yakujadiliwa.

Mwisho wa kumnukulu. Makamu huyo war ais wa Marekani anatarajiwa kuyaweka wazi malengo muhimu ya Marekani katika suala la amani nchini Iraq.

Atakutana na waziri mkuu Nuri al Maliki na mawaziri wake wa ngazi ya juu pamoja na baraza la rais lenye wajumbe watatu wanaowakilisha madhehebu ya Shia,Sunni na Kurdi.

Huku chama cha Demokratic nchini Marekani kikimtia mkiki rais Bush akubali wanajeshi wa Marekani waondoke nchini Iraq,makamu war ais Dick Cheney bila shaka yoyote ataiweka wazi kwa Iraq kwamba hakuna tena cha kungoja ngoja kwa serikali ya Iraq kuchukua juhudi imara za kumaliza machafuko.

Maafisa wa Marekani wamezidi kuzungumzia kero zao juu ya mwendo wa pole wa utungwaji sheria muhimu ikiwa ni pamoja na juhudu za kuweka utaratibu wa kugawana mapato ya mafuta pamoja na kuwaruhusu wanachama wa cha Baath cha aliyekuwa rais wa nchi hiyo Saddam Hussein,kuchukua nyadhifa serikalini.

Baada ya kukutana waziri mkuu al Maliki na bwana Cheney watakwenda kula chakula cha mchana pamoja na mawaziri wa Iraq wa mafuta,ulinzi,mambo ya nje mambo ya ndani na yule wa fedha na baadae bwana Cheney atakuwa na mkutano na rais Jalal Talabani.

Iraq ni moja ya nchi alizopanga kutembelea makamu huyo war ais wa Marekani atakwenda pia Emarati,Saudi Arabia,Misri na Jordan kwa lengo la kuzitolea mwito serikali za Kisunni kuwashawishi wasunni wachache wa Iraq kujiunga na chakato wa kisiasa nchini humo.

Wakati huo huo hali ya umwagikaji wa damu katika taifa hilo inatia mashaka hii leo watu 19 wameuwawa kwenye mji wa Irbil.

Mshambuliaji wa kujitoa muhanga alijiripua ndani ya lori nje ya ofisi za wizara ya mambo ya ndani katika mji wa wakurdi wa Irbil. Watu wengine 80 wamejeruhiwa. Kundi la al Kaida limehusishwa na shambulio hilo lililosababisha uharibifu mkubwa wa jengo la wizara hiyo ya mambo ya ndani.

Irbil ni mji mkuu wa jimbo la Kurdistan nchini Iraq ambako kwa muda mrefu kumekuwepo na hali ya utulivu kiasi licha ya kuendelea machafuko kwenye maeneo mengi ya Iraq.