1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chibok: Donda lisilopona Nigeria

14 Aprili 2015

Sasa ni mwaka mzima tangu Boko Haram wawateke nyara wasichana 276 wa Kinigeria huko Chibok na mwandishi wetu Jan-Phillip Scholz anasema leo ni siku ya kutia msumari mmoto kwenye donda bichi.

https://p.dw.com/p/1F7UT
Symbolbild Entführungen von Frauen und Mädchen in Nigeria
Picha: picture-alliance/dpa/D. Kurokawa

Ilikuwa ni wiki chache baada ya tarehe 14 Aprili 2014, ambapo magaidi wa Boko Haram waliwateka wasichana hao katika kijiji kidogo cha Chibok, ndipo nilipokaa na mmoja wa baba waliotekwa binti yake. Alinielezea namna ambavyo asubuhi ya mkasa huo alipomchukuwa binti yake kumpeleka skuli kwenye pikipiki yake. Namna bintiye huyo alivyouaga kwa kumuambia: "Ahsante baba. Tutaonana baadaye." Baba huyo akaniambia siku hiyo kuwa hakuwa tena na matumaini tena ya kumuona mwanawe akiwa hai.

Mtu anamueleza nini baba kama huyu ambaye tayari matumaini yake yameshakufa? Sikujua wakati huo, sijui leo baada ya mwaka mzima kupita tangu msiba huo wa Jumatatu asubuhi, muda wa mwisho anapokumbuka kuiona sura ya bintiye ikiwa na bashasha na wawili hao kuagana.

Kauli za matumaini hata kama zimekusudiwa kuwa njema kwa sasa zinaonekana na kubuni na tupu. Mengi yameshasikikana juu ya ukosefu wa uwezo na wa dhamira wa jeshi la Nigeria, kiasi cha kwamba mtu hawezi kuwa na matumaini nalo.

Jan-Philipp Scholz
Jan-Philipp ScholzPicha: DW/M. Müller

Imani kwa rais anayeondoka madarakani, Goodluck Jonathan, ilikuwa ya chini sana. Kiongozi huyu hakuona haja ya kusafiri kwenda kuwafariji wanafamilia waliokuwa wakiomboleza masaibu ya binti zao. Kwake, wazazi hawa hawakuwa na la kutegemea.

Alama ya mapambano na kushindwa

Tangu Aprili 2014, Chibok imekuwa alama ya mambo mawili – moja, ni alama ya kushindwa kwa serikali ya Nigeria kwenye mapigano yake dhidi ya Waislamu wenye siasa kali.

Tangu kutokea kwa tukio hili mwaka mmoja uliopita, zaidi ya wanawake na wasichana wengine 2,000 wametekwa na kundi hilo la kigaidi, kwa mujibu wa ripoti ya shirika la haki za binaadamu la Amnesty International.

Ndani ya kipindi hicho, Boko Haram imeshahusika na takribani mashambulizi 300. Kiasi cha watoto 800,000 wanaishi ukimbizini kutokana na mashambulizi hayo, kwa mujibu wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF. Jaala ya watoto hawa haijawahi kupata kuvuma kama ilivyovuma ya wasichana wa Chibok, ambao nao huko kuvuma kwake hakujawasaidia hadi sasa.

Lakini kuna jengine ambalo limeifanya Chibok kuwa alama – nalo ni kuwa kijiji hiki kimekuwa alama ya muamko mpya kwa ulimwengu na kwa raia wa Nigeria. Tangu tukio hilo la Aprili 2014, Nigeria imekuwa si ile tena, imebadilika.

Mtu anaweza kufika umbali wa kusema kwamba kushindwa tena kurudi madarakani kwa Jonathan, kumechangiwa pakubwa na Chibok. Kwa sababu, pamoja na kuongezeka kwa ufisadi katika serikali yake, kulikuwa ni kushindwa kwa Jonathan kukabiliana na magaidi ndiko kulikomuangusha rais huyu anayemaliza muda wake.

Mwandishi: Jan-Phillip Scholz/DW
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman