1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"China iishinikize Myanmar"

Maja Dreyer25 Septemba 2007

Maandamano ya watawa na wananchi dhidi ya serikali ya kijeshi huko Myanmar – hilo ndilo suala muhimu kwenye kurasa za wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

https://p.dw.com/p/CHRl

Mhariri wa “Frankfurter Allgemeine Zeitung” ameandika hivi juu ya matukio ya huko Myanmar:

“Hofu ambayo tangu kuingia madarakani ilikuwa msingi wa mamlaka ya jeshi inaonekana sasa kama inatokomea. Hayo yalitokea katika nchi nyingi tangu mwaka 1989, kwa hivyo majerenali wanaotawala Myanmar wangeweza kuyajua hayo mapema. Lakini kujifunza kutokana na matukio katika historia ni jambo ambalo madikteta wote walishindwa kuelewa. Ndiyo sababu kuna wasiwasi kuwa historia ya aina nyingine itajirudia, yaani kusimamisha maandamano kwa kutumia nguvu. Jeshi la Myanmar linajulikana kuwa halioni haya kuwakandamiza wananchi wake.”

Ni uchambuzi wa mhariri wa “Frankfurter Allgemeine Zeitung”. Mwandishi wa gazeti la “Tagesspiegel” la mjini Berlin anazingatia jukumu la nchi za Magharibi na China katika kuishinikiza serikali ya kijeshi ya Myanmar. Ameandika:

“Ni jambo la kawaida kwa Marekani na nchi za Umoja wa Ulaya kupitia Umoja wa Mataifa kumshinikiza kiongozi wa Myanmar Than Shwe na kudai kutotumiwa njia za kijeshi kutuliza maandamano pamoja na kuanzisha demokrasia nchini humo. Kwa miaka mingi, Marekani na Ulaya zimeiwekea vikwazo Myanmar. Lakini serikali hiyo ya kijeshi haijali vikwazo hivyo, kwa kuwa inaungwa mkono na China. Katika hali kama hiyo shinikizo inabidi iwekwe na nchi ambayo yenyewe ina historia ya kukandamiza demokrasia. Ni miaka 15 sasa tangu mauaji kwenye uwanjwa wa Tiananmen huko China yalipotokea, suali hapa ni: Je, China bado inakubali matumizi ya nguvu ya aina hiyo?”

Mhariri wa “Rhein-Zeitung” pia anaamini China inabeba dhamana kubwa katika suala la Myanmar. Tunasoma:

“Watawa wanaoongoza maandamano na wafuasi wengine hawasaidiwi chochote na uungwaji mkono wa nchi za Magharibi. Ikiwa jumuiya ya Magharibi kweli inataka kuwasaidia waandamanaji basi inalazimika kuishawishi China kubadili sera zake kuelekea Myanmar. Iwapo serikali ya kijeshi huko Rangun itapoteza mshirika wake wa pekee, basi huenda ikalazimika kukubali kushindwa.”

La mwisho tunalinukulu gazeti la “Die Welt” ambalo linatumai kuwa maandamano ya kusaka demokrasia yatafanikiwa.

“Katika hali ambapo jeshi linatawala nchi, kufanya maandamano na kutojali amri ya serikali ni jambo la kuweka maisha hatarini. Kwa kweli ni bahati kubwa kwamba huko Myanmar ni watawa ndio walioingia barabarani, kwa sababu ni vigumu kuwapinga watawa. Na kuwaua watawa hao litakuwa ni kosa kubwa kabisa. Huu ndio msingi wa uhuru wa watawa hao ambao wanawapa moyo wananchi wa Myanmar. Lakini kwa kuanzisha maandamano, watawa hao wa madhehebu ya Kibudda wameanzisha maendeleo ambayo matokeo yake hayajulikani.”