1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China ina maslahi gani barani Afrika?

24 Januari 2007

Mjini Nairobi, Kenya, jukwaa la kimataifa kuhusu masuala ya kijamii duniani linaendelea. Kila siku wajumbe 46.000 kutoka kila pembe ya dunia wanajadili juu ya masuala mbali mbali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Mwandishi wetu Sandra Petersmann alishiriki kwenye warsha kuhusu sera za Uchina kuelekea Afrika ikiwa ni nchi inayozidi kujihusisha kiuchumi barani Afrika.

https://p.dw.com/p/CHlj
Mtaani Chinatown jijini Lagos, Nigeria
Mtaani Chinatown jijini Lagos, NigeriaPicha: AP

Mwanzoni hali ilikuwa ya amani. Watu 300 hivi walikusanyika katika chumba cha warsha hiyo iliyoandaliwa na shirika la “China NGO” ambalo linajiita “mtandao wa ushirikiano wa kimataifa”. Waliohudhuria ni wajumbe kutoka Ulaya na Marekani, lakini hasa ni Waafrika.

Aliyeongea kwanza ni Chen Huifan, mkurugenzi wa jumuiya ya umma wa China ya kupigania amani na upunguzaji wa silaha za vita. Bibi huyu anaelezea sera za China kuelekea Afrika: “Msingi wa kujihusisha kwetu ni ukweli na urafiki, usawa, faida kwa pande zote na ushirikiano. Kwetu sisi urafiki ni muhimu sana na tunataka udumu milele.”

Waliposikia maneno haya wasikilizaji kadhaa walianza kupoteza subira yao. Kule jukwaani bibi huyu aliendelea kueleza juu ya safari yake ya kwenda Ethiopia na vile watoto mabarabarani walivyoshangilia.

Alifurahi sana, anasema Chen Huifan. - Lakini maelezo yake hayakuwafurahisha waliokuwa wakimsikiliza.

Halafu Profesa Isaac Mbeche wa chuo kikuu cha Nairobi akaingilia kati: “Ebu, serikali ya China kweli inataka ushirikiano na nchi za Kiafrika au kunyonya tu rasilimali za bara la Afrika? China inafaa kuwa na sera ambazo zinanufaisha pande zote mbili badala ya kujiendeleza tu wakati Afrika inabaki kuwa maskini.”

Mfano Profesa huyu anaoutoa ni ule wa Zimbabwe ambapo China inachimbua rasili mali kwa kutumia wafanyakazi wa Kichina na rais Mugabe anapata silaha. Umma wa Zimbabwe lakini haunufaiki. Joto lilizidi katika chumba cha mkutano kwenye uwanja wa Moi Kasarani, mjini Nairobi. Halafu katibu mkuu wa shirika hilo la Kichina, Cui Jianjun, akaongea wazi: “Ikiwa hatutakuja hapa, wengine watakuja. Mmeona nchi za Magharibi kutega uchumi kwa miaka mingi, na bado nyinyi ni maskini!”

Halafu hasikiki tena. Berilengar Dathol wa kutoka Tschad anatoka nje. Bwana huyu anahudumia wakimbizi kutoka Darfur waliovuka mpaka. Anasema: “Sababu ya kutokuwa na majeshi ya Umoja wa Mataifa kuhakikisha amani Darfur ni China kupinga. Ikiwa unataka kuiwekea Sudan vikwazo, basi lazima kukubaliana kwanza na China. China inaiunga mkono Sudan, kwa sababu wanachimbua mafuta huko. Na kwetu Tschad ni hivyo hivyo.”

Wajumbe wengi wa mkutano wa Nairobi wanasikitishwa na China na kusema kwamba nchi hii ni sawa na nchi za Magharibi. Wote wanataka tu bidhaa na rasili mali kutoka Afrika kwa bei nafuu, lakini Afrika haipati faida yoyote.