1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China kuimarisha uchumi na jeshi

Mohamed Dahman5 Machi 2007

Waziri Mkuu wa China Wen Jiabao leo amefunguwa kikao cha kila mwaka cha bunge kwa wito wa kuimarisha uchumi endelevu na pia kuahidi kulifanya jeshi la China kuwa na nguvu kubwa. Mohamed Dahman na taarifa kamili juu ya ufunguzi wa kikao cha bunge la China.

https://p.dw.com/p/CHIx
Waziri Mkuu wa China Wen Jiabao
Waziri Mkuu wa China Wen JiabaoPicha: AP

Mbele ya takriban wajumbe 3,000 katika Ukumbi Mkuu wa Wananchi mjini Beijing Waziri Mkuu huyo wa China Wen Jiabao amewasilisha repoti ya kila mwaka ambayo imelenga katika kuuwekea uwiano uchumi wa China ambao umeongezeka maradufu katika kipindi cha miaka minne iliopita.

Wen amesema wanapaswa kuepuka kupigania tu ukuaji wa haraka wa uchumi na kutowa wito wa kuchukuliwa kwa juhudi kubwa za kutunza mazingira baada ya China kushindwa kutimiza shabaha yake ya kuboresha ufanisi wa nishati na utowaji wa hewa chafu zenye kuathiri mazingira hapo mwaka jana.

Wen amesema lazima waweke umuhimu mkubwa katika kuhifadhi nishati,rasilmali na uchafuzi mbaya sana wa mazingira.

Pia Wen amekiri kwamba maslahi ya wananchi wa kawaida yamekuwa yakitolewa muhanga katika mashindano ya kutafuta utajiri ambapo ametaja hatua za kupunguza pengo linalozidi kukuwa kati ya matajiri na maskini hususan katika miji inayoendelea kuwa ya kisasa na maeneo ya vijijini.

Amesema lazima waweke wananchi mbele kabla ya kila kitu,kufanya kazi kwa nguvu kulinda haki katika jamii na sheria na kuhakikisha kwamba wananchi wote wanafaidika na matunda ya mageuzi na maendeleo.

Wen amesema China itaendelea kuimarisha majeshi yake ya ulinzi katika matamshi ambayo yameshangiriwa na viongozi wa kijeshi ambao wanataka zana za kupambana na vitisho vipya na kuichukuwa tena Taiwan watakapotakiwa kufanya hivyo.

Serikali ilitangaza hapo jana kwamba bajeti ya kijeshi kwa mwaka 2007 itaongezeka kwa asilimia 17.8 kutoka mwaka jana na hadi kufikia dola bilioni 45.

Miongoni mwa wajumbe wa kikao hicho cha bunge ni maafisa wa kijeshi wakiwa na mavazi kamili ya kijeshi na wakionekana kuwa na furaha sana na matamshi ya Wen na ongezeko la bajeti.

Waziri Mkuu huyo wa China kadhalika amezungumzia suala la rushwa katika serikali ambayo Rais Hu Jintao ameonya kuwa ni mojawapo ya vitisho vikubwa kwa uhalali wa chama cha Kikomunisti kama chama tawala.Amesema kuna serikali za mitaa na maafisa wa serikali ambao hushindana kwa ufahari na matumizi ya ovyo jambo ambalo limezusha chuki kubwa ya wananchi.

Tuna shida katika kuijenga dola.Tutatowa kipau mbele katika kushughulikia masuala ya ubadhirifu na matumizi mabaya,urasimu na umengi meza katika baadhi ya idara za serikali pamoja na umaskini uliokithiri.Viongozi wanatumia vibaya madaraka yao na kula rushwa.Tukiwa na dhamana kwa dola na wananchi tutachukuwa hatua kali na hatutowavunja moyo wananchi.

Katika mojawapo ya mageuzi makubwa kabisa kuwasilishwa kwenye kikao hicho cha bunge ambacho katu hakikuwahi kukataa pendekezo linalowasilishwa na chama cha Kikomunisti Wen amesema sheria itakayokomesha viwango vya kodi ya upendeleo kwa makampuni ya kigeni itapitishwa.