1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China kujenga kituo cha kuhudumia manowari zake Pembe ya Afrika?

30 Desemba 2009

Afisa mwandamizi katika jeshi la wanamaji la China amependekeza kuwa na kituo cha kudumu, kuhudumia meli zake zinazoshiriki katika ujumbe wa kupiga vita uharamia katika Ghuba ya Aden.

https://p.dw.com/p/LHKi
Manuary ya Uchina yawaandama maharamia katika Ghuba la AdenPicha: picture-alliance/ dpa

China ina manowari zinazopiga doria katika Ghuba ya Aden tangu mwaka mmoja uliopita. Lengo ni kuzisindikiza na kuzilinda meli zake na za nchi zingine dhidi ya mashambulio ya maharamia wa Kisomali. Lakini ni vigumu sana kulinda njia zinazotumiwa na meli za shehena nje ya pwani ya Afrika ya Mashariki. Kwa mfano, meli ya Kichina De Xin Hai iliyokuwa na shehena ya makaa ya mawe ilitekwa nyara mwezi wa Oktoba kiasi ya maili 700 mashariki ya Somalia. Meli hiyo na wafanyakazi wake 25 waligombolewa Jumapili iliyopita baada ya maharamia kulipwa kama dola milioni 4.

Sasa ndio afisa mmoja mwandamizi katika jeshi la wanamaji la China, Admirali Yin Zhuo, amependekeza kuwa na kituo cha kuwahudumia wanamaji wake katika kanda hiyo. Amesema, hilo ni suala linalohusika na siasa za wizara ya mambo ya nje, lakini anaamini ni jambo la maana kwa China kuwa na kituo cha kudumu, kuhudumia manowari zake zinazopiga doria katika pwani ya Afrika ya Mashariki. Ameelezea matatizo yanayovumiliwa na manowari hizo katika jitahada ya kuwapiga vita maharamia.

Manowari za kwanza za China zilibakia baharini siku 124 bila ya kutia nangá ko kote. Lakini baadae manowari zilizopokea zamu ziliruhusiwa kutia nanga na kupata huduma katika kituo cha jeshi la wanamaji la Ufaransa. Hata Marekani, Umoja wa Ulaya na Japan zina vituo vinavyohudumia wanamaji wake wanaoshiriki katika operesheni za kupiga vita uharamia katika pwani ya Pembe ya Afrika.

Admirali Yin, alie pia mkurugenzi wa kamati ya China inayoshauri njia za kuboresha teknolojia ya mawasiliano katika jeshi la wanamaji, anaamini iwapo China itajenga kituo cha kudumu, nchi zitakazokuwa karibu na kituo hicho na hata zile zinazoshiriki katika operesheni ya kupiga vita uharamia, hazitopinga. Yin hakushauri wapi pa kujenga kituo hicho, lakini siku ya Jumanne gazeti la "China Daily" lilichapisha mahojiano yaliyofanywa pamoja na Balozi wa Somalia nchini China. Yeye ameomba msaada wa kimataifa kujenga kituo kitakachosaidia kulinda usalama katika eneo la mwambao.

Lakini China inakodolewa macho na majirani wake barani Asia. Nchi hizo zinatazama kwa makini, iwapo operesheni za China ulimwenguni na kuongezeka kwa hadhi yake, kutaifanya China kuwa na usemi mkubwa zaidi katika masuala ya kimataifa.

Mwandishi: Martin,Prema/RTRE/AFPE

Mhariri: Othman, Miraji