1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China na Marekani zatofautiana Lima

14 Desemba 2014

Shutuma zilihanikiza katika mazungumzo ya mazingira ya Umoja wa Mataifa mjini Lima Jumamosi(13.12.2014),wakati Marekani imeonya kwamba kushindwa kufikia maridhiano kutalizika jukwaa hilo la kimataifa lililodumu miaka 22.

https://p.dw.com/p/1E3rZ
Lima - COP 20
Rais wa Peru Ollanta Humala akihutubia mkutano wa mazingira mjini LimaPicha: Reuters/E. Castro-Mendivil

Mkutano ukiendelea hadi katika siku ya 13 ambayo haikupangwa, majadiliano yaliingia katika mkwamo baada ya kutokea mvutano kati ya mataifa tajiri na masikini kuhusu kugawana majukumu ya kupunguza gesi zinazoharibu mazingira.

Karibu kwa siku nzima baada ya muda uliopangwa wa kufunga mkutano huo, wenyeviti wa makundi ya kufanyiakazi yaliyopewa jukumu la kuandika waraka, waliwasilisha kwa wajumbe wa majadiliano mapendekezo ya maridhiano.

Climate Change Conference COP 20 Lima
Wanawake katika ufunguzi wa mkutano huoPicha: Reuters/Enrique Castro-Mendivil

China na Marekani zavutana

Mataifa mengi tajiri yameukubali kama mwongozo unaowezekana kufanyia kazi. Lakini mataifa yanayoendelea yameutupilia mbali, yakisema waraka huo umeshindwa kuweka mlingano katika hatua za kupambana na utoaji wa gesi zinazoharibu mazingira kwa kuzisaidia nchi zenye uchumi dhaifu.

Mjumbe wa Marekani Todd Stern amesema mkwamo unayaweka makubaliano yanayotarajiwa mwaka 2015 ya mabadiliko ya tabia nchi, pamoja na hali ya kuaminika ya mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadikliko ya tabia nchi, ikiwa ni sehemu ya mkutano wa dunia wa Rio wa mwaka 1992, katika hali ya wasiwasi.

"Kila kilichopatikana hadi sasa kitakuwa hatarini, na kila tunachotarajia kukifikia kitakuwa hatarini pia," Stern amewaambia wajumbe. "Mafanikio ya mkutano huu wa COP hapa mjini Lima yako hatarini," amesema, akitumia neno la kitaalamu kwa ajili ya mkutano huo wa kila mwaka wa makundi mbali mbali.

UN-Klimakonferenz in Lima 13.12.2014
Mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi ukiendelea mjini LimaPicha: AFP/Getty Images/C. Bouroncle

"Mafanikio ya mkutano wa mwaka ujao wa COP mjini Paris yako mashakani na nafikiri mustakabali wa mkutano wa UNFCCC kama chombo cha kujadili mabadiliko ya tabia nchi kwa ufanisi katika kiwango cha kimataifa pia yako mashakani."

Maridhiano hayajafikiwa

Huku likikabiliwa na mgawanyiko, uchovu na hali inayoongezeka ya msuguano, kundi hilo linalofanyia kazi rasimu limekabidhi kijiti cha kutafuta maridhiano kwa rais wa mkutano Manuel Pulgar-Vidal, waziri wa mazingira wa Peru.

"Twende na tufanyie kazi na tupate muafaka," amewaomba wajumbe wa majadiliano. "Sio wakati wa mapendekezo, ni wakati wa suluhisho, tusaidiane." Wajumbe wa majadiliano mjini Lima ni lazima wafikie makubaliano juu ya utaratibu wa kuelekeza hatua mwaka ujao juu ya kutangaza mapendekezo na ahadi za kupunguza utoaji wa gesi zinazoharibu mazingira kitaifa.

Nchi mbili zinazohusika zaidi na utoaji wa gesi zinazoharibu mazingira duniani zimekuwa zikilumbana Jumamosi(13.12.2014) katika mkutano huo mjini Lima.

China imeuita mswada wa mwisho katika mkutano huo usiotosheleza, wakati Marekani imeyataka mataifa zaidi ya 190 yanayohudhuria mkutano huo kuuidhinisha.

Lima - COP 20 Juan Manuel Santos und John Kerry
John Kerry (kulia) na rais wa Columbia Juan Manuel santos mjini LimaPicha: picture-alliance/dpa/M. Castañeda

Mswada huo wa waraka wa kupunguza utoaji wa gesi zinazoharibu mazingira hauakisi tofauti kati ya mataifa tajiri na yale yanayoinukia kiuchumi, inadai China, ambayo inajihesabu miongoni mwa mataifa yanayoendelea licha ya kuwa inatoa kiasi cha robo nzima ya gesi hizo chafu duniani.

"Tumekwama," mjumbe wa China amesema siku moja baada ya mazungumzo kurefushwa ili kuruhusu muda zaidi wa kufikia makubaliano.

Lima - COP 20 Bundesumweltministerin Barbara Hendricks
Waziri wa mazingira wa Ujerumani Barbara Hendricks mjini LimaPicha: picture-alliance/dpa/J. Karita

Mkuu wa ujumbe wa Marekani katika majadiliano hayo, wakati huo huo, amekubaliana na vifungu kadhaa vya waraka huo, lakini pia amesema Marekani inapinga vifungu kadhaa ndani ya waraka huo. Amedai kuwa mafanikio ya mkutano wa Lima sio tu yananing'inia katika mzani lakini pia yale ya mkutano wa Paris mwishoni mwa mwaka 2015.

Makubaliano ya kihistoria kuepusha mabadiliko ya tabia nchi yanatarajiwa kutiwa saini katika mkutano huo.

Mwandishi: Sekione Kitojo/dpae/afpe

Mhariri: Elizabeth Shoo