1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China na Taiwan zakutana rasmi kwa mara ya kwanza

11 Februari 2014

China na Taiwan leo(11.02.2014) zimefanya mazungumzo yao ya kwanza ya kiserikali tangu nchi hizo kutengana miaka 65 iliyopita baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe ikiwa ni hatua muhimu ya kihistoria kwa mahasimu hao.

https://p.dw.com/p/1B6ff
Bilaterale Gespräche zwischen China und Taiwan
Mjumbe wa Taiwan akizungumza na waandishi habariPicha: picture-alliance/dpa

Mkutano huo ni ishara lakini tu lakini ni hatua muhimu ya kihistoria baina ya mahasimu hao wakubwa wa zamani.

Wang Yu-chi kutoka Taiwan , ambaye anahusika na sera za kisiwa hicho kuelekea China, alikutana na mwenzake wa China Zhang Zhijun mjini Nanjing katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku nne.

Huku kukiwa na masuala nyeti muhimu, chumba cha mkutano kilipambwa katika hali ya kawaida , hakuna bendera zilizoonekana na majina hayakuwapo katika meza ya mazungumzo kama ilivyokawaida kuwatambulisha wajumbe, ama hata vyeo vyao.

Wang Yu-chi
Wang Yu-chi mjumbe wa China katika mazungumzo hayoPicha: picture-alliance/dpa

Kabla ya kuondoka , Wang aliwaambia waandishi habari: "Ziara hii haikuwa rahisi, ni matokeo ya mahusiano kati ya pande hizi mbili ya miaka kadha."

Mji wa kihistoria

Nanjing , mji ulioko kusini mwa China , ulikuwa mji mkuu wakati nchi hiyo ikitawaliwa na chama cha Kuomintang, ama chama cha kizalendo, katika nusu ya kwanza ya karne ya 20.

Waliposhindwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, ambapo mamilioni ya watu waliuwawa, dhidi ya chama cha kikomunist cha Mao Zedong mwaka 1949, waungaji mkono milioni mbili wa kiongozi mzalendo Chiang Kai-shek walikimbilia katika kisiwa cha Taiwan, ambacho rasmi kinajulikana kama jamhuri ya China.

Chen Yunlins Besuch auf Taiwan
Wajumbe wa China na Taiwan katika chumba cha mazungumzoPicha: AP

Kisiwa hicho pamoja na China bara zimekuwa kila kimoja na utawala wake tangu wakati huo, pande zote mbili zikidai kuwa serikali halali ya China na zimerejesha mawasiliano katika miaka ya 1990 kupitia mashirika yasiyo rasmi.

Mkutano wa leo ni matunda ya juhudi za miaka kadha za kuleta hali bora ya uhusiano.

Lakini maafisa wa chama cha kikomunist nchini China bado wanalenga kuiunganisha China yote chini ya utawala wao, na wanaiona Taiwan kuwa jimbo lililoasi linalosubiri kuunganishwa tena na China bara, kwa nguvu kama ikilazimika.

Katika miongo kadha Taiwan imekuwa zaidi imetengwa kidiplomasia , na kupoteza kiti cha China katika Umoja wa Mataifa mwaka 1971 na kushuhudia nchi kadha zilizokuwa zikiitambua zikipungua. Lakini inapata silaha kutoka Marekani na imekuwa ikipata maendeleo ya muda mrefu kiuchumi.

Hakuna ajenda rasmi iliyotolewa kwa ajili ya mazungumzo hayo, ambayo kwa kiasi kikubwa yanaonekana kuwa ya ishara tu, na zoezi la kujenga hali ya kuaminiana.

Malengo tofauti

Taiwan inaonekana kulenga kupata matokeo ya maana kutoka katika mazungumzo hayo, kama vile kupata faida za kiuchumi ama uhakika wa usalama, wakati China jicho lake moja liko katika muungano na kisiwa hicho, wanasema wadadisi wa masuala ya kisiasa.

Hatua hii ya kulegeza msimamo wa kisiasa inakuja baada ya pande hizo mbili kupiga hatua za tahadhari kuelekea mapatano ya kiuchumi katika miaka ya hivi karibuni.

Taiwan Straße Manöver
Meli za kivita za China katika ujia wa maji wa TaiwanPicha: AP

Kama warithi wa serikali ya zamani ya China, chama tawala cha Kuomintang nchini Taiwan kinakubali hoja ya msingi ya China moja na inapinga nia ya kutaka kuwa huru kwa kisiwa hicho.

Juni mwaka 2010 Taiwan na China zilitia saini makubaliano ya msingi ya mfumo wa ushirikiano wa kiuchumi , makubaliano ambayo yanaonekana kuwa hatua kubwa hadi sasa ya kukaribiana.

Mwandishi: Sekione Kitojo/afpe

Mhariri: Mohammed Khelef