1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China na uwekezaji wake barani Afrika

15 Juni 2007

China tofauti na nchi nane tajiri duniani G8 mnamo miaka ya hivi karibuni inawekeza moja kwa moja katika miradi ya maendeleo barani Afrika.

https://p.dw.com/p/CHkY
Rais Hu Jintao wa China
Rais Hu Jintao wa ChinaPicha: AP

China, nchi inayoinukia kuwa miongoni mwa nchi zenye nguvu duniani kiuchumi inawekeza moja kwa moja katika miradi ya miundo mbinu kwa mfano ujenzi wa barabara,reli na hata uzalishaji nishati ya umeme kwa kutumia mabwawa swala linaloleta utata.

Tofauti na misaada inayotolewa na nchi za magharibi China inatoa mikopo bila ya masharti jambo ambalo watetezi wa mazingira na wa haki za binadamu wanaelezea kuwa linatia wasiwasi na kwamba huenda China ikaangamiza jitihada zao za kukinga mali asili na pia haki za jamii.

Ilikuwa shangwe nderemo na hoi hoi wakati China ilipokamilisha mradi wa mabwawa matatu ya Gorges katika mto Yangtze mwaka jana.

Maafisa waliusifu mradi huo na kusema kuwa ni mfano jinsi gani mwanadamu alivyo na uwezo dhidi ya nguvu za asili lakini Peter Bosshard mkurugenzi wa maswala ya mazingira wa shirika la kimataifa la matandao wa mito lenye makao yake mjini California nchini Marekani anasema kuwa kitendo China ilichofanya katika mto Yangtze ndio sawa na kutaka kueneza uharibifu wa nguvu za asili katika maeneo mengine duniani hasa barani Afrika.

Kutokana na utalaamu huo wa kiteknolojia China sasa itajenga bwawa la Bui nchini Ghana ambalo loinahofiwa kuwa litadidimiza sehemu za msitu wa nchi hiyo.

Miradi mingine ya uzalishaji wa umeme katika mabwawa inaendelea nchini Nigeria, Zambia, Msumbiji na pia nchini Sudan.

Katika maeneo ya juu ya mto Nile kaskazini mwa Sudan makampuni ya China yanajenga mradi mkubwa kabisa wa uzalishaji umeme barani Afrika katika bwawa la Merowe, mradi huo unaogharimu kiasi cha dola milioni 540 unadhaminiwa na benki ya China inayoshughulika na biashara ya uingizaji na utoaji.

Ujenzi huo lakini unakabiliwa na upinzani mkubwa nchini Sudan, kama anavyo eleza Ali Askouri muwakilishi wa wakulima wanaoathirika na mradi huo katika wa bwawa la Merowe.

Bwana Askouri anasema kuwa wakulima wa kawaida wanathiriwa na mradi wa bwawa la Merowe na kwamba China inafanya inachukuwa mfumo wa kichwa chini miguu juu katika mtazamo wa maendeleo.

Serikali ya China inakanusha vikali shutuma hizo alipoulizwa juu ya mradi huo wa bwawa la Merowe la huko nchini Sudan msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China bibi Jiang Yu alitetea sera za serikali yake kuhusu Afrika.

Wakati huo huo mfumo wa misaada bila vipingamizi vingi wa China unapendelewa na nchi nyingi za Afrika.

Makamu wa rais wa China Wu Yi alipofungua mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi kuhusu China na Afrika mwaka uliopita, mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi kutoka nchi 40 za Afrika.

Kwa mujibu wa waziri wa mambo ya nje wa Sierra Leone Momodu Koroma, nchi nyingi za Afrika zilihudhuria mkutano huo ili kutafuta uhusiano wa karibu na China aidha kuomba mikopo zaidi pamoja na misaada mingine.